Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limewataka wahitimu wa kidato cha sita mwaka 2021 kuhudhuria mafunzo kwa mujibu wa sheria katika kambi walizopangiwa  kuanzia Juni Mosi hadi 10, 2021.

Kaimu mkuu wa utawala wa JKT,  Kanali Hassan Mabena amezitaja kambi wanazotakiwa kuwasili ni Rwamkoma Mara, Msange Tabora, Ruvu Pwani, Mpwapwa, Makutupora Dodoma, Mafinga Iringa, Mlale, Itaka Songwe, Luwa, Milundikwa Rukwa, Nachingwea Lindi na Kibiti Pwani.

Kambi nyingine ni Oljoro JKT Arusha, Mgambo, Maramba Tanga, Makuyuni Arusha, Bulombora  na Mtabila Kigoma.

Kanali Mabena amesema wahitimu wenye ulemavu wa kuonekana kwa macho waripoti katika kambi ya Ruvu JKT iliyopo Mlandizi mkoani Pwani ambayo ina miundombinu ya kuwahudumia.

“JKT linawataka vijana wote kuripoti wakiwa na vifaa mbalimbali ikiwemo bukta za dark bluu, fulana ya kijani, raba za michezo rangi ya kijani au bluu, shuka mbili za kulalia rangi ya bluu bahari na soksi ndefu nyeusi,” amesema.

Aidha amewataka vijana hao pia kuwa na nguo za kuzuia baridi, trakisuti ya kijani au bluu na nauli ya kwenda kambini na kurudi nyumbani.

Limao kupunguza hatari ya kiharusi
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Mei 23, 2021