Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali itahakikisha inawasaka watu wote waliohusika na upotevu wa mali za kiwanda cha chai cha Lupembe na kuwachukulia hatua, na Serikali haitoipa nafasi migogoro yote ya uwekezaji inayopelekea wananchi kutopata ajira bali itatatuliwa bila ya kusimamisha uzalishali.
Majaliwa amesema hayo leo Januari 25, 2017 wakati alipotembelea kiwanda cha chai cha Lupembe akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Njombe, ambapo amewataka wawekezaji mbalimbali waliomilikishwa viwanda wahakikishe wanafuata kanuni na sheria ili kufikia malengo yaliyokusudiwa na wananchi waweze kupata tija.
“Migogoro yote inayopelekea watu kutopata ajira haitapewa nafasi. Tutaisikiliza na kuipatia ufumbuzi bila ya kusimamisha uzalishaji,.. Ushirika nchini uliyumba na umekuwa ukiharibiwa na waliopewa dhamana na ndiyo sababu tuliamua kuufumua uongozi kuanzia juu na tutashuka hadi chini,” amesema.
Amesema Serikali itaendelea kufuatilia viongozi wa vyama vya ushirika na wenye uwezo wa kuviendesha wataendelea na wasioweza wataondolewa.
Pia amesema kuwa Serikali itahakikisha mwenye haki anapata haki yake na haitakubali kuona kiwanda hicho kikisimamisha uzalishaji. Pia inafuatilia muwekezaji huyo alipataje kiwanda.
“Lupembe ni miongoni mwa viwanda ambavyo vilikufa na sasa kimeanza uzalishaji hatutakubali kife kutokana na migogoro ya wanaushirika na muwekezaji. Kiwanda hakitasimama ng’o,”
Aidha, Majaliwa amemtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuja na kufanya uchunguzi wa kiwanda hicho, kwani Serikali imedhamiria kuwaletea wananchi maendeleo na haitamvumilia mtu atakayevuruga uendeshaji wa viwanda. “ Tunataka viwanda vifanye kazi”