Mkurugenzi mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula Duniani (WFP), David Beasley ameitaka mamlaka ya Tigrayan kurejesha mara moja akiba ya mafuta yaliyoibiwa kwa jumuiya ya kibinadamu.
Beasley ameyasema Jumatano ya Agosti 26, 2022 na kudai kuwa kundi la watu wenye silaha waliingia katika ghala la WFP lililopo maeneo ya Mekelle na kukamata kwa nguvu meli 12 zilizojaa zaidi ya lita nusu milioni za mafuta.
Amesema, “Mafuta haya yalikuwa yamenunuliwa na WFP hivi majuzi na yalifika siku chache kabla ya kuibwa na bila mafuta hayo haiwezekani kwa WFP kusambaza chakula, mbolea, madawa na vifaa vingine vya dharura kote Tigray.”
Ameongeza kuwa, ni jambo la kusikitisha kwamba mamilioni ya watu watasukumwa zaidi kwenye njaa kwa kuzuka tena kwa mapigano katika eneo la Kaskazini mwa Ethiopia.
Hata hivyo, Beasley amesema,”Tukio hilo linatuzuia kuwasha jenereta na kutembeza magari, na ili WFP na washirika wa kibinadamu waweze kukidhi mahitaji ya watu wa Tigray wanaoishi katika mazingira magumu, ambapo wastani wa watu milioni 5.2 wanakabiliwa na njaa kali.
Katika miezi michache iliyopita, makubaliano ya kibinadamu yameruhusu WFP na washirika wake kufikia karibu watu milioni 5 huko Tigray na kupotea kwa mafuta haya kutasukuma jamii za Tigray, ambazo tayari zinakabiliwa na athari za vita, kuelekea kwenye janga la njaa.