Wachezaji wa klabu bingwa Tanzania bara (Simba SC) ambao walisalia jijini Dar es salaam, leo wameondoka kuelekea Unguja, kwa ajili ya kujiungana wenzao waliotangulia visiwani zanzibar kwa ajili ya michuano ya Kombe la Mapinduzi.
Msafara wa baadhi ya wachezaji hao umefanyika, baada ya kikosi cha Simba kutinga hatua ya nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi, kwa kuifunga Zimamoto FC mabao matatu kwa moja, kwenye mchezo wa mtoano uliounguruma jana kwenye uwanja wa Gombani Pemba.
Kwa mafanikio hayo Simba SC itacheza dhidi ya Azam FC, na iwapo itafanikiwa kushinda basi huenda ikakutana na Young Africans au Mtibwa Sugar katika fainali ya Kombe la Mapinduzi.
Azam FC ambao ni mabingwa watetezi wa michuano ya Kombe la Mapinduzi walifanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo kwa mwaka huu, baada ya kuifunga Mlandege bao moja kwa sifuri, juzi Jumatatu.
Simba SC iliamua kuwaacha nyota wake wote waliocheza katika mchezo dhidi ya Young Africans, huku ikiwatumia wachezaji wa akiba na wale wa kikosi cha vijana katika mchezo wa kwanza ya Kombe la Mapinduzi.
Simba SC inajua ugumu wa mchezo wao wa nusu fainali dhidi ya Azam FC inayonolewa na Aristica Cioaba ambao ndiyo mabingwa watetezi.
Mchezo huo unakuwa wa kulipa kisasi katika fainali za Mapinduzi baada ya mwaka jana Azam kuifunga Simba 2-1 na kuchukua kombe hilo.
Simba na Azam FC zitacheza nusu fainali ya pili Ijumaa huku nusu fainali ya kwanza ikichezwa Alhamis kati ya Yanga dhidi ya Mtibwa Sugar na michezo yote ikichezwa kwenye Uwanja wa Amaan, Unguja.
Wakati huo huo kikosi cha Simba kilichoshinda mchezo wa jana dhidi ya Zimamoto FC kimewasili mjini Unguja kikitokea Pemba, tayari kwa mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya Azam FC.