Jeshi la Polisi mkoani Arusha linawashikilia vijana watatu wenye umri kati ya miaka 20 hadi 26 wakazi wa mkoani humo kwa kosa la kuwadanganya wananchi wanaohitaji kuunganishiwa umeme kwamba wanaweza kuwapatia huduma hiyo kwa njia ya mkato kwa kuwa wao ni maofisa wa TANESCO.
Akitoa Taarifa hiyo leo Agosti 18, 2021, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha ACP Justine Masejo, amesema kuwa watuhumiwa hao walikamatwa Agosti 17, 2021, katika ofisi za TANESCO zilizopo Mtaa wa Old Line, Kata ya Themi, Halmashauri ya Jiji la Arusha.
Aidha watuhumiwa hao ni pamoja na Gidion William (26) ambaye ni mkazi wa Sombetini, Richard Frank (20) mkazi wa Daraja II pamoja na Godson Erick (20), mkazi wa Moshono.
Kamanda Masejo amesema jeshi hilo linaendelea kuwahoji watuhumiwa hao ili kuupata mtandao mzima unaohusika na vitendo hivyo vya kitapeli katika ofisi za Shirika la Umeme la TANESCO mkoani humo.