Watu 45 wamepoteza maisha katika kijiji kimoja jimbo la Kaduna nchini Nigeria baada ya watu wenye silaha kuvamia kijiji hicho na kuchoma moto nyumba.
Wahanga wa tukio hilo wengi wao wanadaiwa kuwa ni wale wa kundi maalum lililoundwa kwa lengo kulinda mifugo kijijini hapo kufuatia matukio kadhaa ya wizi.
Imeelezwa kuwa watu hao wenye silaha walizingira kijiji cha Gwaska majira ya mchana na kuanza kurusha risasi hovyo huku wakichoma moto nyumba. Kila aliyetaka kutoroka alishambuliwa vikali, kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na BBC.
Serikali ya Rais Muhammadu Buhari imeendelea kulaumiwa kwa kile kinachodaiwa kutochukua hatua za kuridhisha kusitisha vitendo hivyo vya kihalifu vinavyochukua maisha ya wananchi wasio na hatia.
Mwezi uliopita, wachimbaji wadogo wa madini 14 waliripotiwa kuuawa na watu wenye silaha katika eneo la Birnin Gwari.