Mahakama ya Venezuela imewahukumu kifungu cha miaka 20 jela watu wawili waliowahi kuwa Makomando wa Jeshi la Marekani, baada ya kuwatia hatiani kwa kufanya jaribio la kumpindua na kumteka Rais wa Venezuela, Nicolás Maduro.

Luke Denman (34) na Airan Berry (41) pia walikutwa na hatia ya kushirikiana kufanya uhalifu, kuingiza silaha nzito nchini humo kinyamela na ugaidi.

Denman na Berry walikuwa miongoni mwa watu 13 waliokamatwa, Mei mwaka huu wakijaribu kuingia kwa njia haramu nchini Venezuela wakitokea Colombia.

Mwanasheria Mkuu wa Venezuela, Tarek William Saab amesema kuwa taratibu za kisheria zitaendelea dhidi ya watu wengine waliokuwa nao, wanaotuhumiwa kuwasaidia kufanya uhalifu huo.

Saad ameweka picha inayoonesha magari, silaha na nyaraka za utambulisho kwenye mtandao wa Twitter na kuandika, “watu wa Marekani wamekamatwa na wamekiri kuwa walihusika kufanya haya.”

Rais wa Marekani, Donald Trump ambaye ni mpinzani wa utawala wa Serikali ya Rais Maduro amekana kuhusika na vitendo vilivyofanywa na wanajeshi hao wa zamani.

Marekani inamuunga mkono kiongozi mkuu wa upinzani nchini Venezuela, Juan Guaidó na inamtambua kama kiongozi halali wa nchi hiyo.

Mapema mwaka huu, Denman na Berry ambao walikuwa makomando wa Marekani, walionekana kwenye video iliyorushwa na Televisheni ya Venezuela.

Katika video hiyo, walikiri kuhusika katika oparesheni ambayo wanadai waliipa jina la ‘Oparesheni Gideon’, iliyokuwa na lengo la kumuua Rais Maduro au kumteka na kumpeleka nchini Marekani.

Kwa mujibu wa BBC, Berry alieleza kuwa alikodiwa kwa ajili ya kuendesha mafunzo ya kijeshi kwa raia wa Venezuela nchini Colombia kabla ya kurudi Caracas, wakiwa na lengo la kudhibiti uwanja wa ndege ili kumruhusu Rais Maduro kuondolewa nchini humo.

Denman alisema yeye na mwenzake Berry walikodiwa na kampuni ya ulinzi iliyoko Florida inayofahamika kama Silvercor USA, kwa ajili ya kutekeleza oparesheni hiyo. Mmiliki wa Kampuni hiyo, Jordan Goudreau ambaye pia ni askari mstaafu wa Jeshi la Marekani amekiri kuhusika na oparesheni hiyo.

Washington Post imechapisha nyaraka inayoonesha kuwa mkataba kati ya makomando hao wa zamani na kampuni ya Silvercor USA ulikuwa na thamani ya $213 milioni, kwa kuivamia Venezuela na kumpindua Rais Maduro.

Rais Maduro amekaririwa akimtuhumu moja kwa moja Rais Trump kuwa alikuwa nyuma ya oparesheni hiyo, lakini kiongozi huyo wa Marekani amekanusha vikali tuhuma hizo dhidi yake.

Waziri Mpango: PPRA wanafanya kazi nzuri, waongeze elimu kwa umma

Watoto wafariki wakiwa wamelala, mama aliwasha jiko la mkaa kupata joto

JPM: Nataka tuwauzie Ulaya mitumba
Waziri Mpango: PPRA wanafanya kazi nzuri, waongeze elimu kwa umma