KAtika hali isiyokuwa ya kawaida, Wapendanao wawili waliokuwa wafungwa zamani wamefunga pingu za maisha katika sherehe iliyoandaliwa kwenye Gereza la King’ong’o, kaunti ya Nyeri nchini Kenya.

Virginia Karondu mwenye umri wa miaka 24 na Martin Mzera, 28, walikula viapo vya ndoa Jumanne, Machi 1, katika uwanja wa gereza hilo kuwatia moyo wafungwa wenzao wa zamani kuwa wanaweza kupata mapenzi baada ya kufungwa.

Karondu alisema alikutana na Mzera akiwa jela na hakuamini anaweza kupata penzi akiwa mfungwa.

“Jela ni kama nyumbani nilikutana na mpenzi wangu hapa. Nilipokutana na Mzera, sikuwa tayari kuolewa kwa sababu sikuamini kwamba angetaka kuolewa na mfungwa wa zamani, lakini nilimpenda zaidi baada ya kuchumbiana na kufahamiana,” Karondu alisema.

Kulingana na Karondu, alifungwa jela kwa miaka saba kwa sababu ya kupatikana na bangi na kujaribu kuua. “Nimekuwa mfungwa kwa miaka saba. Nilifungwa katika jela la vijana nikiwa na umri mdogo. Baada ya kumaliza masomo yangu ya sekondari nilafaa kupelekwa jela la wanawake Langata lakini hakimu alinihurumia na kuachilia huru,” alieleza.

Mzera alitumikia kifungo cha mwaka mmoja jela baada ya kumaliza masomo yake ya sekondari kwa kujiunga na genge la uhalifu. “Nilifungwa jela baada ya kujiunga na genge lililotoka kuwaibia watu lakini nilikuwa na bahati kwamba hakimu alikuwa na huruma kwangu,” alisema.

Mzera, alifungwa gerezani mwaka 2015, ambako alipitia programu ya International Youth Fellowship na kuachiliwa huru mwaka 2016 huku barafu wake wa moyo, Karondu naye akiachiliwa huru mwaka wa 2017.

Hata hivyo wakati wa sherehe ya ndoa hiyo, wafungwa zaidi ya 380 walihitimu na kutunukiwa vyeti vya Elimu ya Mindset na Theolojia.

Serikali yasema hakuna muda wa ziada fedha za UVIKO-19
Dkt. Kijaji ataja sababu za kupandishwa bendera ya Tanzania Burj Khalifa