Serikali inafanya uchunguzi kuhusu uhusika wa maafisa wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) kwenye sakata la upigaji wa Sh28.5 bilioni kupitia zabuni ya mradi wa mfumo wa utambuzi wa mamlaka hiyo.
Hatua hiyo imewekwa wazi na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango alipokuwa akifungua Mkutano wa Kimataifa wa Manunuzi ya Umma (IPPC) ulioanza rasmi jana jijini Arusha. Dkt. Mpango amesema kuwa maafisa watakaokutwa na hatia ya kushiriki katika mchezo mchafu kwenye tenda hiyo kwa lengo la kuiba fedha za umma watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Sakata hilo liliwekwa wazi siku chache zilizopita baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola kuwataka walioshinda zabuni hiyo ya Sh28.5 bilioni na kisha kutotekeleza mkataba huo warejeshe fedha hizo. Baadhi ya wazabuni walianza kujitokeza kurejesha.
Dkt Mpango aliahidi kuwa hatua ya kuwashughulikia watumishi wa umma waliohusika iko palepale, na kwamba fagio hilo litapita kwenye manunuzi ya umma yote nchini.
Alisema kuwa Mamlaka ya Manunuzi ya Umma kupitia ripoti yake ya Mwaka wa Fedha 2017/18 iliweka wazi jinsi ambavyo taasisi nyingi zilisababisha hasara au watumishi wake kujihusisha na uvunjifu wa sheria ya manunuzi. Hivyo, Dkt Mpango alisema kuwa vyombo vingine vya uchunguzi vinaendelea na kazi yake ili kuhakikisha waliohusika “wanacheza nyimbo walizoziimba wenyewe.”
Makampuni saba yalishinda zabuni ya mfumo wa utambuzi wa Nida, lakini hayakutekeleza mkataba husika. PPRA ilifanya uchunguzi maalum mwaka 2016 na kuwasilisha ripoti yake.