Ndugu wa raia wa Rwanda aliyekuwa mmoja kati ya watu 157 waliokufa kwenye ajali ya ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia aina ya Boeing 737 Max, wameiburuza mahakamani kampuni ya Boeing iliyotengeneza ndege hiyo.

Ndege hiyo iliyokuwa ikisafiri kutoka Addis Ababa, Ethiopia kuelekea Nairobi nchini Kenya ilianguka dakika sita baada ya kuruka, mapema mwezi huu.

Familia ya Jackson Musoni, imeeleza kuwa imeamua kuishtaki Boeing kwani imebaini uzembe wa watengenezaji wa chombo hicho ndio chanzo kikuu cha ajali iliyochukua uhai wa ndugu yao, kwa mujibu wa BBC.

Boeing imekumbwa na misukosuko ya kusakamwa kwa kushindwa kusimamia ipasavyo utengenezaji wa ndege pamoja na uendeshaji wake kwa marubani, baada ya kutoa toleo jipya ambalo ndani ya miezi mitano tu ndege mbili mpya zimeanguka na kuua mamia ya watu.

Jana, Boeing ilieleza kuwa imefanyia marekebisho mifumo yote ambayo ilikuwa ikitajwa kuwa huenda ndio chanzo cha ajali za ndege mbili za Boeing 737 Max.

Uchunguzi wa ajali hizo bado unaendelea na matokeo yake yanasubiriwa huku kampuni ya Boeing ikiwa imeingia hasara kubwa pia kibiashara kutokana na ndege zake kususiwa.

Video: Wasanii Dumila walivyoupokea Mradi wa TACIP kwa kishindo
Video: NASSARI kulipa FIDIA Bunge baada ya kushindwa Mahakamani? | "Spika ametekeleza maagizo..."