Watu wawili waliotoka gerezani hivi karibuni kwa msamaha wa Rais wameuawa baada ya kukamatwa wakidaiwa kuiba vitu mbalimbali huko kwa Mathiasi mjini, Kibaha mkoani Pwani.

Watu hao walifungwa kwa makosa ya wizi katika kesi ya jinai namba 273/2020 na 260/2020 na walitoka kwa msamaha wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, uliotolewa Aprili 26 mwaka huu, kutoka katika gereza la Mkuza mjini Kibaha.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Wankyo Nyigesa amesema leo Mei 10, 2021 kuwa watu hao wameuawa Mei 8 alfajiri kwa kupigwa na mawe, mapanga na fimbo na wananchi wenye hasira waliowatuhumu kuhusika kwenye tukio la wizi.

“Hawa watu wametambuliwa ni Ramadhani Mohamed maarufu kwa jina la Seven au Ali (28)  mkazi wa kwa Mathiasi na Idd Hamisi maarufu Chuga (30) mkazi wa mtaa Jamaika, wote walikuwa wamerudi uraiani hivi karibuni kwa msamaha wa Rais,” amesema Nyigesa.

Hata hivyo, Kamanda Nyigesa ameshauri wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi kwa kisingizio cha hasira na badala yake watoe taarifa polisi inapotokea tukio la wizi kwenye maeneo yao, ili watuhumiwa wakamatwe na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Marekani yapitisha sheria ya dharura bomba la mafuta
Sudan Kusini: Rais Salva Kiir avunja Bunge