Mahakama nchini Rwanda imewafunga jela watu 15 waliokutwa na hatia ya kujihusisha na makundi ya kigaidi ya Islamic States of Iraq and Syria (ISIS) na Al-Shabaab.
Kupitia hukumu hiyo iliyosomwa jana, 13 walihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela kila mmoja na wawili walihukumiwa kifungo cha miaka miwili jela kila mmoja.
Mahakama hiyo pia iliwaachia huru watu 25 baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha bila kuacha shaka kuhusu mashtaka yaliyokuwa yanawakabili.
Polisi wa Rwanda waliwakamata watu hao 40 Januari 2016 ikiwa ni wiki moja tu tangu kuuawa kwa Muhammad Mugemangango, mhubiri maarufu aliyetuhumiwa kuwahamasisha vijana kujiunga na makundi ya kigaidi.
Vyombo vya usalama pia vilikamata vitu vilivyodaiwa kutumika kusambaza mtazamo na mawazo ya kigaidi kwa vijana kama CD, vitabu pamoja na baadhi ya wamiliki wa akaunti za mitandao ya kijamii.
Kati ya watu 15 waliohukumiwa kifungo, watatu ni wanawake na wawili kati yao walikamatwa wakiwa Uwanja wa Ndege wakielekea nchini Syria na mmoja alidaiwa kuwapa $1,000 kwa ajili ya tiketi ya ndege.