Ikiwa yamesalia masaa machache kabla ya kuwasili kwa Mfalme wa Uingereza Charles III Nchini Kenya, Wazee wa jamii ya Wamasai wameshinikiza kurejeshewa ardhi wanayodai, ambayo wanadai walipokonywa wakati wa vita vya kujitafutia uhuru Taifa hilo.
Mwenyekiti wa jamii hiyo, Mzee Kelena Olenchoy amesema Wazee hao wanadai ekari takribani milioni 700 waliyopokonywa wakati wa vita vya kudai uhuru, ambayo ilikuwa inatumiwa na Waingereza kuendeleza shughuli za biashara ikiwemo mbuga binafsi za Wanyama na Kilimo.
Kwa niaba amesema, “ipo baadhi ya miji ambayo japo ilikuwa yetu wanaoishi hapo ni Wakenya, hiyo hatutaki kurejeshewa ila tulipwe fidia. Lakini ardhi inayotumiwa na Waingereza kwa sasa kufuga wanyama turudishiwe pamoja na hao wanyama maana ni wetu.”
Aidha, Mzee Olenchoy ameongeza kuwa, wao wanadai fidia kutokana na madhila waliyopitia wakati wa vita hivyo na pia msamaha wa hadharani wa Mfalme wa Uingereza Charles III huku pia wakituma ombi la kutaka kufanya mazungumzo na Mfalme huyo wakati wa ziara yake nchini Kenya, la sivyo wataelekea Mahakamani kudai haki.
Mfalme Charles III na Malkia Camilla, wanatarajiwa kuzuru Kenya kati ya Oktoba 31 – Novemba 3, 2023 ikiwa ni ziara yake ya kwanza katika mataifa ya jumuiya wa madola, tangu kutawazwa kuwa Mfalme mapema mwaka huu wa 2023.