Serikali imewaonya wamiliki wa Vituo vya kulea watoto nchini, kuacha kujinufaisha na misaada ya kifedha inayotolewa na wahisani na kwamba kama wameshindwa kuviendesha wa watoe taarifa kwa Maafisa wa Ustawi wa Jamii popote walipo katika maeneo yao, ili watoto hao wapate sehemu nyingine watakazopata malezi.

Onyo hilo, limetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. John Jingu mara baada ya kutembelea Kijiji cha Matumaini kinachowalea watoto jijini Dodoma na kuongeza kuwa, baadhi ya wamiliki wa Makao ya kulea watoto wamekuwa wakifanya hivyo na hata kupiga picha za watoto kwa ajili ya kupata misaada ambayo haiwafikii walengwa.

Amesema, “mnaotumia Makao ya Watoto kujinufasha tunawamulika, tutawafuatilia na tutawachukulia hatua kali kwa sababu mnakiuka Sheria na taratibu zilizopo. Huu ni wizi na ukatili dhidi ya Watoto na tunawahujumu waliotoka hiyo misaada.”

Aidha, Dkt. Jingu ameongeza kuwa watoto wanatakiwa kulelewa na kutunzwa katika familia na jamii na inapotokea mtoto amepata changamoto za maisha na kujikuta yupo katika mazingira ambayo anakosa Malezi Makao kama hayo hutumika kuwalea.

“Mpaka sasa kuna jumla ya Makao ya kulea watoto 341 ambayo yanatoa huduma ya kulea watoto waliopatwa na changamoto zilizosababisha kutolelewa katika familia, nasisitiza kuzingatia suala la Malezi hasa katika tamaduni na maadili ya kitanzania ili kujenga watoto walio na maadili mema hivyo kujenga taifa lenye maadili,” amesema Dkt. Jingu.

Gamondi achimba mkwara Young Africans
CR Belouizdad yamng'oa Simon Msuva