Serikali imewataka waajiri na wamiliki wa Vyombo vya habari nchini kuwaajiri waandishi wa habari kwa mikataba maalumu ambayo inampa mwandishi nafasi ya kuingia katika mifuko ya kijamii na kuweza kuruhusiwa kuwa chini ya sheria na sera zote za ajira ikiwa ni pamoja na kujiunga na Vyama vya wafanyakazi ili kupunguza migogoro na changamoto ambazo zinawapata waandishi na kusababisha kazi zao kufanyika kwa kiwango cha chini.

Hayo yamesemwa na Kamishna wa kazi, Suzan Mkangwa, katika Kikao cha wadau wa sekta ya Habari cha mashauriano kuhusu utekelezaji wa Sheria za kazi kilichofanyika mkoani Dodoma Februari 16, 2022.

Amesema kuwa waajiri wengi wanakwepa kuwaajiri kwa mikataba maalumu waandishi wa habari kwa kuwa wanakwepa kuwapa waandishi malipo au mishahara iliyoainishwa kisheria na kukwepa kufuata sheria za kima cha chini cha mshahara ambayo ndio faida ya mwandishi inayobakizwa pia katika mafao yake ya baadae.

“Pamoja na jitihada zote zinazofanywa na serikali katika kuhakikisha kunakua utekelezaji mzuri wa heria za kazi na mazingira mazuri ya kazi, bado kumekuwa na changamoto katika utekelezaji wa sheria hizo ambapo baadhi ya sehemu za kazi hazizingatii sheria, viwango vya kazi za staha kitu ambacho ni kinyume cha haki za binaadamu na misingi ya utawala bora,” amesema Kamishna Mkangwa.

Aidha Kamishna Mkangwa ameongeza “baadhi wa waajiri wameendelea kukiuka matakwa ya sheria za kazi ikiwemo kutotoa mikataba ya ajira, kutowapa haki ya kujiunga na vyama vya wafanyakazi, kutowasajili na kuchangia katika mifuko ya hifadhi ya jamii, kuwaachisha kazi wafanyakazi bila kufuata sheria, pamoja na madai ya mishahara.”

Kamishna wa kazi, Suzan Mkangwa.

Katika kuchangia mada Mwenyekiti wa Chama cha wafanyakazi taifa RAAWU, Jane Mihanji amesema waajiri wengi wa vyombo vya habari hawataki vyama vya wafanyakazi maofisini kwao kwa kuwa wanadhani vyama vikiwepo humo ni chanzo cha migogoro kati yaao na waandishi wao.

“Unakuta mwandishi amemaliza elimu nzuri, lakini anaambiwa aanze kama muwakilishi anaejitolea bila mkataba, hapo hapati stahiki zake kama inavyotakiwa na kuna wakati atapelka habari na kujikuta ile habari yake haijapelekwa hewani hivyo halipwi.” amesema Mihanji.

Kikao hicho kimeandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu kikiwa na lengo la kufanya majadiliano na masahauriano kuhusu utekelezaji wa Sheria za Kazi ili kuimarisha mahusiano mema kati ya waajiri na wafanyakazi na kuongeza ufanisi mahali pa kazi na mgeni rasmi alikuwa ni Katibu Mkuu wa wizara Prof. Jamal Adam Katundu.

Kocha Simba SC aweka imani kwa John Bocco
Kapombe afichua siri ya kukubali kupiga Penati