Taharuki imeibuka katika jiji la Kinshasa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), baada ya wanachama wa chama tawala kuvamia Kanisa Katoliki saa chache baada Serikali kupiga marufuku maandamano yaliyoandaliwa na kanisa hilo kupinga utawala wa rais Joseph Kabila.
Wanachama hao wa People’s Party for Reconstruction and Democracy (PPRD) wanadaiwa kufika kanisani hapo kwa magari ya umma wakitokea maeneo tofauti, wakidai wamefika hapo kusali na kulinda nchi yao, mwishoni mwa juma lililopita.
“Walikuja wakiwa ndani ya sare zao, walikuja kwa mabasi ya umma na walishambulia sehemu ya kuabudia ya Bikira Maria,” muumini aliyejitambulisha kwa jina la Felicite Mbula aliiambia AFP.
Aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo, waliahirisha kufanya ibada ya jioni ambayo ilikuwa maandalizi ya ibada ya jioni.
Aidha, mmoja kati ya viongozi wa kanisa hilo, Antoine Bokoka amesema kuwa wafuasi wa PPRD walikuja wakijidai wanataka kusali lakini haikuwa hivyo.
Serikali ya DRC ilipiga marufuku maandamano dhidi ya utawala wa Kabila baada ya yale yaliyofanyika kwenye mkesha wa mwaka mpya na mengine ya Januari 21 kusababisha watu 15 kuuawa na maafisa wa usalama, kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa.
Maandamano hayo yaliyokuwa yanaandaliwa na viongozi wa dini, yanapinga uamuzi wa rais Kabila kubakia madarakani licha ya muhula wake kuisha kikatiba tangu mwaka 2016.
Tayari Serikali ya rais Kabila imeitisha uchaguzi utakaofanyika mwishoni mwa mwaka huu, lakini wanaompinga wanataka aachie madaraka haraka iwezekanavyo.