Wanafunzi zaidi ya elfu 20 waliokuwa wanapatiwa chakula shuleni na shirika moja la Kijerumani lisilokuwa la kiserikali katika mkoa wa Kirundo kaskazini mwa Burundi wameacha kuhudhuria masomo shuleni.

Viongozi wa elimu katika mkoa huo wamesema kuwa wanafunzi laki moja na nusu wa shule za msingi katika mkoa huo, walikuwa wanapatiwa msaada wa chakula kutoka shirika hilo, kwa kupata mlo shuleni ili wasiache shule baada ya kudhihirika kwamba familia zao zinakabiliwa na umaskini.

Hiyo ikiwa ni moja ya athari ya hatua ya serikali ya Burundi kusitisha shughuli za mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs ) 130 tangu tarehe mosi Oktoba, kwa madai kuwa mashirika hayo ya hisani hayaheshimu sheria mpya inayoongoza shughuli za mashirika ya kimataifa ya kigeni.

Aidha, serikali ya Burundi ilitoa masharti kadhaa kwa mashirika hayo na kuyapa muda wa miezi mitatu ili yawe yamekwisha tekeleza masharti hayo ili yaweze kuendele kufanya kazi.

Baadhi ya masharti hayo, ni pamoja na mashirika hayo ya kigeni kuweka pesa zao zote za matumzi za kigeni kwenye benki kuu ya taifa hilo na kuhakikisha usawa kati ya makabila muhimu ya Burundi wakati wa kuajiri wafanyakazi.

Kwa upande wa wawakilishi wa nchi zinazofadhili NGOs hizo ambazo ni Marekani, Canada, Japan, USwiss, Umoja wa Ulaya na Shirika la Umoja wa Mataifa linalo simamia maendeleo (UNDP), wametoa tamko kwa vyombo vya habari wakiomba kuwepo mazungumzo zaidi na Serikali ya Burundi, ili kupata mwanga na muafaka kuhusu masharti yaliyotolewa.

 

China yaonesha ndege mpya ya kivita inayokwepa rada
Ujerumani kudhamini tamasha la Sauti za Busara