Makumi ya watu, wengi wakiwa ni wanafunzi wa shule ya msingi wanaosoma shule za bweni walitekwa jana Magharibi mwa Cameroon.
Kwa mujibu wa Serikali ya Cameroon, takriban wanafunzi 79 na watu wengine watatu akiwemo mkuu wa shule, walitekwa Jumatatu asubuhi katika jiji la Bameda, Mkoa wa Kaskazini Magharibi.
Msako mkali unaohusisha jeshi la nchi hiyo umeanza huku watuhumiwa wa kwanza wakitajwa kuwa ni kundi la wanajeshi waasi. Eneo hilo limekuwa likishambuliwa na waasi katika miaka ya hivi karibuni.
Gavana wa eneo hilo, Adolphe Lele L’Afrique ameiambia BBC kuwa macho ya vyombo vya usalama yanalimulika kundi la wanajeshi waasi waliojitenga na jeshi la Serikali.
Wanajeshi ambao wamekuwa wakidai uhuru wa aneo la watu wanaozungumza Kiingereza, wamewahi kuitisha mgomo kwa wanafunzi. Lakini hadi sasa hakuna kundi lolote ambalo limetangaza kuhusika na utekaji huo.
Wanafunzi waliotekwa wanatajwa kuwa na umri kati ya miaka 10 na 14.
Video ya watoto ambayo wanaosadikika kuwa ndio waliotekwa na kwamba ilirekodiwa na mmoja kati ya watekaji, imesambazwa kwenye mitandao ya kijamii.