Jeshi la polisi wilayani Kahama mkoani Shinyanga linawashikilia wanafunzi nane wa shule ya sekondari seeke kwa tuhuma ya kumshambulia na kumjeruhi Costantine Makoye mwanafunzi mwenzao majeraha ambayo yamesababisha kufariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya Halmashauri ya Mji Kahama.

Kamanda Abwao amewataja majina ya wanafunzi hao kuwa ni Isaya Athuman (18), Godfrey Fanuel Simon (18), Enock Lazaro Alfred (17), Athuman Azizi (17)  Leonard Emmanuel Lutonja (17), Michael Philipo (17), Sadiki Boniface stephen (18), Emmanuel musa Sekela (18).

Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga ACP Richard Abwao amethibitisha kushikiliwa kwa wanafunzi hao na kusema kuwa tukio hilo limetokea septemba mwaka huu katika kanisa la SDA Wasabato Kahama ambapo kulikuwa na sherehe ya kuwaaga wanafunzi washirika wa kanisa la SDA waliokuwa wakitarajia kuhitimu kidato cha nne.

Amesema Baada ya sherehe hiyo kuisha katika kanisa hilo wakati wanafunzi wanatawanyika alitokea Constantine Makoye akiwa na vijana wenzie wapatao 10 ambao hawajafahamika mara moja na haijulikani kama walikuwa miongoni mwa waalikwa katika sherehe hiyo.

Kamanda Abwao amesema wanafunzi hao walimvamia mwanafunzi aitwaye Isaya Athuman (18) mwanafunzi kidato cha nne seeke secondary, na kutaka kumnyang’anya viatu alivyokuwa amevaa na wengine waliwanyang’anya maji ya kunywa wanafunzi waliokuwa katika sherehe hiyo.

Ndipo wanafunzi hao walipopiga kelele na yowe kwamba wamevamiwa, waliungana pamoja na kuanza kuwarushia mawe hao waliovamia sherehe hiyo na Wavamizi hao walikimbia na kutawanyika lakini Constantine Makoye alizidiwa na kulala chini na wanafunzi hao walimtelekeza hapo.

Amefafanua kuwa Baadae aliamka na kwenda nyumbani kumjulisha Babu yake ambaye alimpeleka kutibiwa katika hospitali ya serikali Kahama bila kutoa Taarifa kituoni hadi alipozidiwa tarehe 01/10/2019 akiwa hawezi kuongea ndipo ndugu walijulisha kituoni na jalada lilifunguliwa kwa kosa la kujeruhi na maelekezo ya mwanafunzi huyo hayakupatikana kutokana na hali yake kuwa mbaya.

Tarehe 02/10/2019 alifariki dunia wakati anaendelea na matibabu Mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi na kubaini chanzo cha kifo ni majeraha makubwa kichwani na wamekabidhiwa Ndugu kwa ajili ya mazishi.

Amesema Chanzo cha Tukio hilo ni madhara ugomvi uliotokana na wanafunzi na watu waliokuwa kwenye eneo la tukio kujichukulia sheria mkononi wakimtuhumu marehemu kuwa mwizi.

Michael Wambura aachiwa huru, aanza kurejesha mamilioni
Mbowe amlilia Mapunda aliyeimba wimbo wa Chadema