Bodi ya mikopo ya elimu ya juu (HESLB) imefunga dirisha la maombi ya mikopo kwa njia ya mtandao kwa mwaka wa masomo 2020/2021 kwa kupokea maombi ya wanfunzi 92, 947.
Serikali kupitia HESLB imetenga shilingi billioni 464 kwa ajili ya wanafunzi 145,000, miongoni mwao wanufaika 54,000 watakuwa wa mwaka wa kwanza na 91,000 ni wanaoendelea na masomo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mkurugenzi mtendaji wa HESLB Abdul-Razaq Badru, mfumo wa maombi hautaruhusu usajili wa maombi mapya ya waombaji isipokuwa waombaji 7500, walipo mtandaoni ambao hawajakamilisha maombi yao.
HESLB ilifungua dirisha la maombi ya mikopo kwa njia ya mtandao kwa siku 40 kuanzia Julai 21 ambapo kwa mujibu wa Badru, kufuatia maoni na maombi ya wazazi bodi iliongeza siku 10 ambazo zimemalizika jana Septemba 10.
“Leo (jana) saa 6:00 usiku dirisha la upokeaji wa maombi ya mikopo kwa wanfunzi wa elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2020/21 kwa njia ya mtandao litafungwa rasmi. Baada ya muda huo usajili mpya kwa ajili ya maombi mapya hautaruhusiwa,” amesema Badru.
Aidha, Badru amesema Oktoba Mosi, HESLB itaanza zoezi la uchambuzi wa maombi hayo na baadaye itaorodhesha maombi yenye mapungufu na kuwatangazia wahusika kwa ajili ya kurekebisha kasoro zilizojitokeza.