Mbunge wa Jimbo la Kibakwe, George Simbachawene amewataka Wanafunzi kuweka bidii katika masomo na kuiachana dhana ya kwamba elimu ya sasa haina umuhimu kwasababu za hata Wasomi nao wapo mtaani wakikosa ajira.
Simbachawene ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ametoa nasaha hizo katika mahafali ya 19 kwa Wanafunzi wa kidato cha nne wa Shule ya Sekondari Rudi, iliyopo Kata ya Rudi, Wilayani Mpwapwa Dodoma.
“Ninawaomba Wananchi wote wa Jimbo la Kibakwe kupitia kwenu ninyi wazazi wa watoto hawa wanaofanya mahafali yao leo, kutambua kuwa mtu aliyemaliza kidato cha nne ana uwezo mkubwa wa kuchambua mambo kisayansi ukilinganisha na yule wa darasa la saba, hivyo elimu ni muhimu,” alisema.
Aidha, Simbachawene ameongeza kuwa, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amelenga kuboresha Sekta ya elimu ili kidato cha nne iwe ni lazima na Wananchi wa Jimbo la Kibakwe watanufaika na maono hayo.