Mamia ya wanafunzi wa shule ya msingi ya St. Anne wameandamana na kufunga barabara ya Jogoo jijini Nairobi nchini Kenya, baada ya basi la abiria maarufu kama ‘Matatu’kumgonga na mtu aliyekuwa akiwasaidia kuvuka barabara.
Kwa mujibu wa Daily Nation, wanafunzi hao wamefunga barabara kuu katika mji mkuu wa nchi hiyo ikiwa pia ni siku chache baada ya kuripotiwa kuwa gari moja lilimgonga na kumuua mwanafunzi mwenzao na kisha kutokomea.
Imeelezwa kuwa wanafunzi hao wameweka mgomo kwa kulala na kukaa barabarani huku wakiweka mawe katika maeneo mengine ya barabara hiyo, wakidai kuwekwa matuta barabarani hapo. “Tunataka haki itendeke kwa mwenzetu, hakuna matuta hakuna kusoma,” wanasikika wanafunzi hao.
Mashuhuda wa tukio la ajali wameeleza kuwa gari hilo lilikuwa likijaribu kulipita kwa kasi gari lingine kabla ya kumgonga mtu huyo aliyekuwa anajitolea kuwavusha wanafunzi.
Vyombo vya usalama vimeingilia tukio hilo na kuahidi kufanyia kazi maombi ya wanafunzi hao, baada ya magari mengi kulazimika kurudi yalipotoka kwa muda mrefu.