Ili kukabiliana na changamoto ya watoto wa kike kukosa masomo, Serikali imeziagiza Halmashauri zote kujenga vyumba vya kujisitiri kwa wanafunzi wa kike mashuleni, ili kuwasaidia kujisitiri wakati wa hedhi.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), David Silinde ameyasema hayo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Santiel Kirumba.
Amesema, ujenzi wa matundu ya vyoo unazingatia mahitaji ya wanafunzi wote wakiwemo wavulana na wasichana pamoja na wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Mbunge Santiel, katika swali lake la nyongeza, aliyehoji juu ya Wanafunzi wa kike ambao wamekuwa wakikosa masomo kwa siku 50 kwa mwaka na kuuliza ahadi ya Serikali katika madarasa mapya ambayo mengi hayana vumba vya kujisitiri.