Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya – DCEA, Aretas Lyimo amesema Wanafunzi wengi wa Shule za Msingi na Sekondari, wamekuwa wakiangukia kwenye matumizi ya Dawa za kulevya kitendo ambacho hupelekea wengi wao kutomaliza masomo yao na kufanikiwa kielimu.
Lyimo ameyasema hayo hivi karibuni wakati alipokuwa akiongea na Dar24 Media jijini Dar es Salaam kuhusu zoezi la utoaji wa elimu kwa jamii juu ya sheria zinazoongoza Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, madhara na aina ya Dawa za kulevya.
Amesema, “wananchi watusaidie katika hili tufanye operesheni kwa pamoja lengo ni kuwapa uelewa wa kutosha ili kuhakikisha wanajiepusha na kupiga vita Dawa za kulevya maana zina athari kubwa sana zinaharibu uchumi wetu, jamii na nguvu kazi ya vijana ambao ndiyo wajenzi wa Taifa.
“Wanafunzi ndio kundi kubwa linaloathirika na Dawa za kulevya wengi wanaingia kwa kutokujua wakiamini kuwa wakivuta au wakivuta Dawa za kulevya au wakivuta bangi basi watasoma zaidi au watakuwa na akili sana au kumudu masomo yao lakini mwisho wa siku wanaanguka.