Wanafunzi wa Shule za Serikali (Kata) Wilayani Bariadi Mkoani Simiyu, Ibrahim Buyungumya kutoka Shule ya Sekondari Nkololo, aliyeongoza kimkoa kwa kupata daraja la kwanza kwa alama saba na Kwandu Maduhu wa Biashara Sekondari aliyepata daraja la kwanza alama kumi na moja, wamekiri kuwa kambi za kitaaluma zimechangia kuongeza ufaulu wao katika Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2018.
Wameyasema hayo katika hafla ya kuwapongeza walimu waliofanikisha na wanafunzi waliofanya vizuri katika Matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha nne mwaka 2018 Kimkoa na kuufanya mkoa kushika nafasi ya Tisa Kitaifa, iliyofanyika katika Shule ya Sekondari Nkololo wilayani Bariadi.
Aidha, wamesema kuwa pamoja na kumuomba Mungu, juhudi zao binafsi za kujisomea, jitihada za walimu, malezi kutoka kwa wazazi wamekiri kuwa kambi za kitaaluma zilizofanyika mkoani Simiyu kwa madarasa yote ya mitihani ziliwasaidia kuwaandaa na mtihani huo wa Taifa.
”Namshukuru Mungu kunifanikisha kupata daraja la kwanza alama saba, nawashukuru walimu wangu, wazazi wangu kwa namna walivyokuwa msaada kwangu, pia kipekee namshukuru Mkuu wetu wa Mkoa, Anthony Mtaka kwa kutuletea kambi zimetusaidia sana,”amesema Ibrahimu Buyungumya pamoja na Kwandu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Biashara, Mathias Joseph ambaye shule yake ilifanya vzuri kwa kupata alama A 23 na alama B 79 amesema pamoja na kambi za kitaaluma siri nyingine ya kufanya vizuri ni jitihada zilizofanywa na walimu pamoja na usimamizi mzuri wa mikakati iliyowekwa na idara ya Elimu na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
-
Wananchi Makambako waishukia Halmashauri kuhusu fidia
-
Zambia yapiga marufuku mifuko ya Plastiki
-
Wodi ya Wazazi Hospitali ya Mpwapwa yazidiwa na Wagonjwa
Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka amewapongeza Viongozi, Walimu, Wanafunzi, Wazazi na Wadau wote wa elimu mkoani humo, kwa jitihada walizofanya katika kuongeza ufaulu.
Jumla ya wanafunzi 7094 kati yao wavulana ni 4224 na wasichana 2875 walifanya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne mwaka 2018 mkoani Simiyu na kuwezesha mkoa kushika nafasi ya tisa Kitaifa kati ya mikoa 31, ambapo umepanda kwa nafasi mbili ikilinganishwa na mwaka 2017 ambapo ulishika nafasi ya 11 Kitaifa.