Wanafunzi wa shule ya sekondari Kwa USO iliyopo halmashauri ya wilaya Bukoba Mkoani Kagera wamenusurika kifo baada ya bweni katika shule hiyo kuteketea kwa moto usiku wa kuamkia julai 30 mwaka huu.

Wakiongea kwa hisia kali wanafunzi hao wameeleza hali waliyokutana nayo baada ya kuona moja ya bweni kati ya mabweni yao likiungua na kusababisha uharibifu wa mali zao ambazo mpaka sasa hazijajulikana thamani yake.

Angel Mulokozi ni mmoja wa wanafunzi ambaye amesema kuwa baada ya kuona tukio hilo la moto alipata mshutuko na kupoteza fahamu kutokana na kukutana na kitu ambacho hakuwahi kukutana nacho katika maisha yake ambapo ameongeza kuwa licha ya hali hiyo wanafunzi wanaendelea vizuri na hakuna aliyeumia.

“Tulikuwa darasani tukijisomea na baada ya kuona kinachoendelea nilipata mshutuko kwakuwa nimeona kitu ambacho sikuwahi kukiona katika maisha yangu ila kwasasa namshukuru Mungu naendelea vizuri na wanafunzi wote waliopata mshutuko kama mimi tunaendelea vizuri.” Ameeleza mwanafunzi Angel.

Angel ameongeza kuwa katika bweni lililoungua hakuna mwanafunzi aliyekuwemo licha ya mali zao kuungua hali iliyosababisha wanafunzi kushindwa kuokoa mali katika bweni hilo.

Hata hivyo wanafunzi hao wameongeza kuwa kutokana na kutokuwemo kwenye bweni hilo kumesababisha kuchelewa kuokoa mali zao na hivyo hasara kubwa kuwakuta.

Kwaupande wake matroni katika shule hiyo ambaye ameongea kwa shariti la  kutotaka jina lake litajwe amesema kuwa yeye alikuwa kwenye moja ya bweni ambalo limetazamana na bweni lililouungua alihamaki baada ya kuona moto umeshakuwa mkubwa licha ya jitihada ya kuzima kushindikana kutokana na uwezo wa wanafunzi kuzima kuwa mdogo.

Matroni huyo ameongeza kuwa wapo wanafunzi ambao walikimbizwa hospitalini  na wengine walipata huduma palepale baada ya magari ya huduma za kwanza kuwasili kwenye eneo la tukio.

Kwaupande wake mkaguzi msaidizi wa polisi na kaimu mkuu wa upelelezi Bukoba Franck Sambaa ameeleza kuwa baada ya kupata taarifa ya ajali hiyo walifika kwenye eneo la tukio kwa kushirikiana na jeshi la zima moto na uokoaji ili kuhakikisha madhara Zaidi hayatokei.

Sambaa amesema kuwa baada ya kufika walianza kuwatoa wanafunzi pamoja na watua ambao walikuwa wameshafika kwenye maeneo ili kuhakikisha mali za wanafunzi zilizookolewa pamoja na mali za shule zinabaki salama.

Aidha afisa operation mkoa wa Kagera Mkaguzi Thomas Majuto akiongea kwaniaba ya mkuu wa jeshi la zima moto na uokoaji amesema kuwa baada ya kupata taarifa za kutokea kwa moto huo walijitahidi kuanza safari ya kwenda kwenye eneo la tukio ambapo wakiwa njiani gari lao lilipata hitrafu na kushindwa kufika suala lililowapelekea kuagiza gari jingine na kufanikiwa kuuzima moto huo ambao tayari ulikuwa umeshateketeza mali za wanafunzi.

Thomas ameongeza kuwa chanzo cha moto huo hakijafahamika na uchunguzi wa moto huo unaendelea licha ya kuwa inasadikika ni shoti ya umeme na kueleza kuwa nje ya mali za wanafuzi kuharibika hakuna madhara yanayohusu binadamu kama kuumia ama kifo.

Shule ya sekondari kwa Uso inamilikiwa na kanisa katoriki jimbo la Bukoba ambayo inatoa elimu kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne.

TASAF yaanza utekelezaji mpango wa kunusuru kaya masikini
Mbaloni kwa kunajisi watoto