Serikali imeshauriwa kusikiliza mapendekezo ya Wadau wa Habari, yanayotaka kurejesha utaratibu wa usajili wa kudumu kwa Magazeti na kuondoa mfumo wa usajili kwa kila mwaka.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya Wananchi, Waandishi wa Habari na wadau wamesema vipo vipengele vya sheria ya huduma ya Habari ya mwaka 2016 vyenye kuhitaji kufanyia marekebisho yatakayosaidia kukuza kwa ufanisi sekta ya Habari nchini.

“Huenda kuna ulazima wa kufanya maamuzi haya ya sheria lakini jambo kubwa la kujiuliza ni matokeo ya sheria yenyewe je? yanaleta matokea ya namna gani kwa muhimili huu muhimu wa Habari,” amesema mmoja wa wadau Ernest Malima.

Kwa upande wake mwanahabari mkongwe Hamza Kasongo amesema kwasasa Dunia ipo kiganjani na kwamba haihitaji macho ya ziada ili kuona umuhimu wa kuweka mazingira rafiki kwenye utendaji wa kazi za vyombo vya Habari hivyo ipo haja ya kufanyia kazi mawazo ya wengi.

Amesema mabadiliko ya vifungu vya sheria katika muhimili wa Habari yanatakiwa kuendana na mazingira husika na kwamba maamuzi yoyote yanapaswa kuzingatia matakwa ya wakati uliopo kwani jambo hilo litasaidia ukuzaji wa sekta ya Habari, pato la Taifa, fursa za ajira na kuishibisha jamii taarifa zenye mashiko.

“Serikali huenda ina nia njema ya utungaji wa sheria au kanuni za usimamizi wa sekta ya habari na huenda inataka kupata matokeo chanya lakini hiyo haimaanishi kuwa hatuwezi kufanya maboresho ya baadhi ya maeneo yenye mapungufu,” amefafanua Kasongo.

Awali mmoja wa walaji wa Habari mwananchi Jackson Malaba  amesema uzingatiaji wa kanuni ni umuhimu lakini mtazamo na maamuzi ya utungaji wa sheria zenyewe unapaswa kuangalia matokeo zaidi madala ya matakwa kwani itasaidia utendaji wa kazi wenye heri baina ya Serikali na vyombo vya habari.

Amesema utungaji wa sheria hufanya na Viongozi ambao ni watu na huelekezwa kwa wahusika ambao ni pia watu hivyo kabla ya kuzipitisha ni vyema wahusika wakajiweka kwenye upande wa pili ili kupata uhalisia na kuona ikiwa ni wao wangeishi vipi kwenye eneo hilo.

“Na hii si katika Habari pekee ni maeneo yote ya sheria maana watunga sera na sheria au kanuni na utaratibu huwa hawana tabia ya kujiweka upande wanaoutungia sheria au kanuni nadhani mmoja wao angefanya hivyo.angeonja ladha halisi na kuwa kinara wa maboresho,” amefafanua Malaba.

Mapema hivi karibuni kulifanyika mkutano wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), uliojikita kuangazia mapendekezo ya mabadiliko ya Sheria ya Habari nchini yaliyowasilishwa serikali.

Sheria hizo ni pamoja na ile ya Huduma ya Habari ya mwaka 2016, Sheria ya Mawasiliano ya Elektroniki na Posta (EPOCA) ya 2010 inayosimamia radio, TV na Mitandao ya Kijamii.

Nyingine ni Sheria ya haki ya kupata Habari ya mwaka 2016 na Sheria ya makosa ya Mtandao ya 2015 zikiwemo na kanuni za maudhui mtandaoni za mwaka 2018 ziliyogawanywa katika vipengele mbalimbali.

Tanzania kuzikabili changamoto soko la ajira
Jeshi lapanga kutawala miezi 24