Serikali imeshauriwa kufanya mapitio katika baadhi ya vifungu vya mapendekezo ya mabadiliko ya Sheria ya Habari nchini, na kuangalia utaratibu wa utoaji leseni za magazeti kutoka mfumo wa kila mwaka na kurudisha ule wa usajili wa kudumu.

Ushauri huo umetolewa na wadau wa Habari kufuatia marejeleo ya mjadala unaoendelea katika sekta hiyo nchini juu ya umuhimu wa kurekebisha sheria na kufuta neno “kwa kudhamiria” linavyovizunguka vifungu vya sheria vyenye mapungufu.

Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina kwa maslahi ya kikazi, mmoja wa Waandishi wakongwe nchini amesema yapo mambo mengi yanayopaswa kutazamwa kwani baadhi ya sheria zinatengeneza mazingira ya rushwa kitolea mfano suala la idara ya Habari Maelezo kupewa madaraka na Sheria katika kifungu cha 5 (l) kuratibu matangazo yote ya Serikali.

“Kuna neno jingine eti kwa kudhamiria sasa hii si sawa, ifikie kipindi Serikali ielewe inatengenezea Sheria wakati gani, Hayati Rais Mstaafu Mkapa aliwahi kusema hizi ni zama za uwazi na ukweli haina kufichana vifungu vilivyoainishwa vina mapungufu ya wazi na zama zimebadilika,” amesema Mwandishi Huyo.

Naye Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Youth Pride Network East Afrika (YPN-EA), Amandus Dominic amesema si vibaya kuangalia mapungufu yanayopigiwa kelele na wahusika ambao ni vyombo vya Habari, kwani wana elewa mazingira wanayoyaishi katika tasnia ikiwemo kujua mahitaji yao.

“Mfano unafungia Gazeti, pale unaharibu mfumo mzima wa maisha ya watu na familia zao ambao walikuwa na ajira pale, unasimamisha uzalishaji ina maana hakuna kinachoingia unategemea unapokuja kulifungua huyu mtu anatoa wapi pesa za uendeshaji? hii haijakaa sawa,” amefafanua Dominic.

Amesema, “Maamuzi mengine ni ya kukomoa kama si kufelishana maana hali ilivyo kila jambo linapaswa kufanyiwa kazi kirafiki na hii ni kwa sekta zote si Habari pekee, sasa yale magazeti waliyafungia je ilileta picha gani zaidi ya kuua Uhuru wa tasnia ya Habari? waliangalie jambo hili.”

Vifungu vinavyotajwa kuwa na mapungufu katika sheria hiyo ni pamoja na kile cha 4 (1), 5 (1), 6(1),7(1), 7(3), 9, 11, 22(1) na 22(2), ikiwemo kuondolewa kwa kifungu kinachompa Mkurugenzi wa Idara ya Habari madaraka ya kuratibu matangazo yote ya serikali.

Mapema Juni 2022, Jukuwaa la Wahariri Tanzania (TEF), kupitia Mkutano maalumu uliofanyika kwa njia ya mtandao lilijadili mapendekezo ya Mabadiliko ya Sheria ya Habari nchini, wakipendekeza utaratibu wa zamani ambapo gazeti lilikuwa linasajiliwa na kujiendesha bila kufutwa kama ilivyo sasa.

Vitambilulisho vya NIDA kulipiwa Elfu 20
KKKT Konde mgogoro usioisha, Polisi yaingilia