Waandishi wa Habari nchini, wametakiwa kutambua umuhimu wa nafasi waliyonayo na kuitumia vyema katika kuielimisha jamii juu ya dhana pana ya Kidiplomasia.
Rai hiyo, imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula wakati akifungua mafunzo ya uandishi wa Habari za Kidiplomasia jijini Dar es Salaam Julai 27, 2022.
Amesema, Waandishi wana nafasi kubwa ya kuilinda na kuitetea taswira ya Tanzania kupitia kazi zao na kuwataka kuzingatia taswira uandishi unaolenga kulinda maslahi ya nchi.
“Tambueni kuwa mna nafasi kubwa ya kujenga taswira ya nchi kwa uandishi unaozingatia masuala ya uelimishaji jamii kuhusu mambo ya Kidiplomasia hivyo umakini unahitajika na ni lazima kuwa wazalendo,” amesema Balozi Mulamula.
Aidha, amesisitiza juu ya suala la kozi fupi kwa Waandishi juu ya masuala ya Kidiplomasia uwe ni endelevu, ili kufanikisha uoatikanaji wa taarifa sahihi katika jamii kupitia vyombo vya Habari.
Katika mafunzo hayo ya siku mbili yanayofanyika Chuo cha Diplomasia kilichopo eneo la Kurasini, Balozi Mulamula pia amewataka watendaji wa Wizara ya mambo ya Nje kuhakikisha wanaimarisha mahusiano kati yao na vyombo vya Habari.
“Tuendelee kushirikiana na vyombo vya Habari maana hawa ni wadau muhimu, tufanye kazi pamoja kwa manufaa ya Taifa, hii ni nchi yetu sote, taswira yake ikiharibika basi ni sisi tumehusika,”
Awali, akiongea katika mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Mawasiliano Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga amesema Wizara itaendelea kuratibu mafunzo hayo ili kusaidia kuboresha uandishi wa masuala ya Kidiplomasia.
Mafunzo hayo ya siku mbili, yaliyoandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki yanalenga kuwajengea uelewa Wanahabari mambo mbalimbali ikiwemo Itifaki, Diplomasia ya umma, Uzalendo na Mawasiliano ya kimkakati baina ya Tanzania na Mataifa Duniani.