Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameoa wito kwa wanahabari kuzingatia miiko na kanuni za kimaadili zinazoongoza taaluma hiyo na kuweka kipaumbele kwenye ustawi wa Taifa badala ya maslahi binafsi.
Amesema kuwa wanahabari wanapaswa kutambua kuwa habari ni bidhaa ya jamii na siyo bidhaa ya kuuzwa hivyo wanawajibika kwa umma na wanapaswa kutetea maslahi ya Taifa.
Amesema hayo wakati alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan katika Hafla ya Utoaji Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT).
“Wanahabari wenye weledi na wanaozingatia maslahi ya Taifa ni chachu ya kutimiza dhima ya kuleta mchango kwa taifa.”amesema Majaliwa.
“Haiba na taswira yenu nzuri huwa inaharibiwa na uandishi wa habari usiofuata maadili ya uandishi wa habari, kuandika habari ambazo hazijafanyiwa utafiti, kuandika habari za uongo na za kupotosha zenye lengo la kuichafua Serikali au mtu mmoja mmoja”
Ameongeza kuwa vitendo hivyo ni kinyume na kanuni za maadili ya taaluma yenu zinazowataka kutafuta ukweli wa habari kabla ya kuzitangaza na kuepuka kutoa taarifa za uongo zilizopikwa kwa lengo la kudanganya umma, kupotosha ukweli au zenye nia ya uchochezi.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ametoa wito kwa waandishi wa Habari wa Tanzania kushiriki kwa kuwasilisha kazi zao za habari katika kuwania tuzo za kimataifa kutokana na kazi nzuri wanazofanya ndani ya nchi.