Wanaharakati wanaopinga mapinduzi nchini Sudan wameitisha maandamano makubwa leo Jumapili, wakati maafisa wa afya wakisema idadi ya watu waliouwawa imefikia 40.
Marekani na Umoja wa Afrika zimelaani ukandamizaji dhidi ya waandamanaji na kuwataka viongozi wa Sudan kujizuia na matumizi ya nguvu.
Chama cha wanataaluma wa Sudan SPA, kimewataka raia kuendeleza maandamano.
SPA ni mwavuli wa vyama vilivyoongoza maandamano yaliyosababisha rais Omar al Bashir kuondolewa madarakani mwaka 2019.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat amezitaka mamlaka za Sudan kurejesha utaratibu wa kikatiba na kipindi cha mpito cha kidemokrasia kulingana na makubaliano ya 2019 ya kugawana madaraka kati ya jeshi na raia.
Nayo kamati ya kuwalinda waandishi wa habari imetoa wito wa kuachiwa huru waandishi wa habari waliokamatwa wakati wakiripoti maandamano ya kupinga mapinduzi.