Wanajeshi 100 wa Umoja wa Afrika pamoja na waangalizi 100 wa haki za binadamu wamepelekwa nchini Burundi kusaidia juhudi za kulinda amani nchini humo kufuatia machafuko yanayoendelea.

Taarifa zilizotolewa na Umoja wa Afrika zimeeleza kuwa Rais Pierre Nkurunzinza ameridhia kupelekwa kwa wanajeshi hao nchini kwake, baada ya kufanya mazungumzo na ujumbe wa maraisi watano wa Afrika waliingia nchini humo wakiongozwa na Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma.

Ujumbe huo wa Marais wa Afrika umefanya ziara ya siku mbilini nchini humo na kufanya mazungumzo na Rais Nkurunzinza pamoja na wapinzani wake wawili kwa lengo la kutafuta muafaka na kurejesha amani nchini humo.

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni ambaye ndiye mpatanishi wa Burundi aliyeteuliwa na Umoja wa Afrika anatarajia kuanzisha mazungumzo na pande zote nchini humo hivi karibuni.

Awali, Rais Nkurunzinza alipinga mpango wa Umoja wa Afrika kupeleka wanajeshi nchini humo bila ridhaa yake akieleza kuwa endapo wanajeshi hao wataingia nchini humo atatambua hatua hiyo kama uvamizi.

Machafuko nchini Burundi yalianza mwezi Aprili, baada ya Nkurunzinza kutangaza kuwa angegombea urais kwa muhula wa Tatu, akidaiwa kuvunja katiba ya nchi hiyo inayotaja ukomo wa mihula miwili.

Walimu kuanza kupanda daladala Bure
Mkutano Mkuu wa ZFA waazimia Mazito, Viongozi watumbuliwa 'Jipu'