Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa Nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo – MONUSCO, kimetangaza kuchukuwa hatua kali dhidi ya Wanajeshi wake wanaotuhumiwa kwa makosa ya utovu wa nidhamu ikiwemo unyanyasaji wa kingono.
Kwa mujibu wa MONUSCO, imeeleza kuwa walinda amani wanane waliokuwa mjini Beni, mashariki mwa Kongo, walikamatwa Oktoba Mosi, 2023 na mmoja alisimamishwa kazi wiki moja baadaye kwa tuhuma za unyanyasaji kingono na mashambulizi.
Wanajeshi hao tisa, wote ni kutoka Afrika Kusini na huenda wakawa wanahusika na uvunjaji ulioenea wa kanuni za Umoja wa Mataifa kiasi cha kupelekea kuchukuliwa hatua hizo na mamlaka za juu zinazoshughulikia Nidhamu.
Hata hivyo, taarifa iliyotolewa na MONUSCO imeeleza kuwa tayari Maafisa hao wameanza kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sera ya kutokuvumilia utovu wa nidhamu, ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa – UN, Antonio Guterres.