Wakazi wa kijiji cha Mgazini, wilaya ya Songea, mkoani Ruvuma wameiomba serikali kupitia Wakalawa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura) mkoani humo kutenga fedha za kutosha ili kukarabati na kujenga barabara ambazo zitapitika majira yote ya mwaka.
Wakizungumza kwenye mkutano uliowashirikisha wajumbe wa shirika lisilo lakiserikali la Roa chini ya Mradi wa Mfumo wa Ufuatiliaji wa Uwajibikaji katika Jamii (SAM) Wananchi hao wamesema wakati umefika serikali kuboresha barabara zilizosahaulika kwa muda mrefu ili waweze kusafirisha mazao yao kwenda sokoni.
Mbali ya kusafirisha mazao, pia barabara hizo zitasaidia kuepuka usumbufu kwa wagonjwaambao wanatakiwa kuwahishwa katika vituo vya afya na hospitali kupata matibabu.
Mmoja wa wananchi hao, Mpendane Soko amesema katika kijiji cha Mgazini kuna zahanati ndogo ambayo wakati mwingine inakabiliwa na wingi wa wagonjwa na wanapotaka kwenda kituo cha afya Lugagala wanashindwa kufika kwa wakati kutokana na ubovu wa barabara inayounganisha kijiji hichona Lugagala.
“Tukifika Lugagala tunalazimika kwenda hadi kijiji cha Muungano Zomba ndipo tupate usafiri wakwenda Lugagala hivyo kuongeza gharama kubwa ya maisha, ni barabara fupi ambayo ingekuwamsaada kwetu lakini kwasasa haipitiki kirahisi hata kwa boda boda kutokana na ubovu,” amesema.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Tarura Halmashauri ya Songea Vijijini, Simon Binamu amesema wapo katika mchakato wa kutafuta fedha ili kukarabati barabara hiyo.
“Kazi zetu zinategemea sana fedha kwa hiyo tunafanya mchakato wa kutafuta fedha na mara tukipataharaka sana tutaifanyia kazi kwani nimefika na nimeiona kimsingi ni kweli inahitaji matengenezo,” amesema Binamu.