Baada ya kutangazwa chanzo cha ugonjwa usio julikana ulioibuka katika kata za Maruku na Kanyangereko, Halmashauri ya Bukoba Mkoani Kagera kuwa ni Marburg, Serikali kupitia idara ya afya kwa kushirikiana na viongozi wa kisiasa na wananchi wameanza mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

Mkuu wa Wilaya ya Misenyi, Kanali Wilson Sakulo ameyasema hayo wakati akihutubia kwenye kilele cha maadhimisho ya wiki ya maji ambapo Wilaya ya Misenyi ambayo yamefanyika katika kijiji cha Kabyaile, kata ya Ishozi na kuwataka wananchi kufuata maelekezo yanayotolewa na wataalam na kuchukua tahadhari.

Mkuu wa wilaya ya Misenyi, Kanali. Wilson Sakulo akitoa maelekezo kwa wananchi kujihadhari na ugonjwa wa Marburg kwenye kilele cha wiki ya Maji duniani.

Amesema “naomba tuendelee kuchukua tahadhari tuhakikishe tunaacha tabia zetu za kusalimiana tunapeana mikono tufate maelekezo ya wataalam wa afya na sambamba na wiki ya maji mhakikishe mnanawa mikono kwa maji tiririka kwa manufaa yenu na haya maji yalete tija kwetu ili tuendelee kuhakikisha tunamtua mama ndoo kichwani.”

Naye Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera, Dkt. Isesanda Kaniki amesema, “hatua mbalimbali zimeanza kuchukuliwa ikiwa timu zote zimeanza kufatilia sehemu husika kwenye mialo, vijijini na sehemu za kutolea huduma, utoaji elimu kuhusiana na ugonjwa lakini pia ufatiliaji endapo mtu akishabihiana na dalili za ugonjwa huo na kwa mwananchi ukijisikia dalili fika mapema kwenye kituo cha afya.”

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Isesanda Kaniki akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hatua wanazochukua dhidi ya ugonjwa wa Marburg.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Misenyi, Justus Tegamaisho amewasisitiza wananchi kuendelea kufatilia taarifa za ugonjwa wa Marburg na kunawa mikono kama sehemu ya kujikinga na magonjwa ya milipuko na kudai kuwa “zile taratibu tulizokuwa tunafata kipindi cha mlipuko wa uviko 19 zianze kufatwa upya, sasa mabadiliko ya kujilinda katika familia zetu urudi pale pale.”

Akisoma taarifa ya utekelezaji miradi ya Mwaka huu, Meneja wa Wakala wa Maji safi na mazingira Vijijini – RUWASA, Endrew Kirembe wakati amesema tayari miundombinu ya maji katika wilaya ya Misenyi imefikia asilimia 75 huku ikiwemo kituo cha kuwapokea wagonjwa wa magonjwa ya milipuko cha Kabyaile kilichopo katika kijiji cha Kabyaile tayari nacho kimeshapata maji.

Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Kabyaile kata ya Ishozi waliohudhuria hafla ya kilele cha wiki ya maji.

Amesema, “tulitekeleza agizo lako la kupeleka maji kwenye kituo cha afya ambacho kipo Kabyaile, kituo chetu muhimu sana cha afya kwahiyo maji yameshafika mpaka pale na wananchi ambao wako kwenye kijiji hiki na wao tumewapelekea huduma na tunaendelea kuwapelekea huduma.”

Kutokana na serikali kuteua kituo cha Kabyaile kuwapokea wagonjwa wa magonjwa ya mlipuko ikiwemo wa Marburg, Wananchi wa kijiji cha Kabyaile wamesema wameanza kuchukua hatua ikiwemo kufuata maelekezo ya wataalam ambapo hadi sasa jumla ya watu wanane wamekutwa na changamoto ya ugonjwa wa Marburg na watano kati ya wamepoteza maisha na hakuna taarifa mpya ya kuongezeka kwa wagonjwa wala kifo.

Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Machi 23, 2023
Simbachawene ataka elimu mapambano dhidi ya Kipindupindu