Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka Viongozi mkoani Singida kuwa na mikakati ya kutumia fursa za kiuchumi badala ya kujikita kwenye sekta moja tu ili kuongeza kasi ya maendeleo ya mkoa huo.
Rais Samia ametoa tamko hilo wakati akihutubia wananchi katika maadhimisho ya miaka 60 ya mkoa huo yaliyofanyika katika uwanja wa Bombadia na kuwataka viongozi kuwahamasisha wananchi kupanda mazao yanayostahamili ukame pamoja na kutumia mbegu bora na za muda mfupi.
Amesema, Wananchi wanatakiwa kulima mazao ya alizeti, dengu na ufuta ambayo hustawi katika maeneo mengi ya mkoa wa Singida pamoja na zao la korosho ambalo pia linafanya vizuri katika maeneo mengi ya mkoa huo, huku akiiagiza Wizara ya Kilimo kuhakikisha miradi ya umwagiliaji inatekelezwa katika maeneo yote yaliyobainishwa kwa ajili ya ujenzi wa skimu.
Awali, Rais Samia alizindua daraja la Msingi lenye urefu wa mita 100 lililopo Wilaya ya Mkalama ambalo limegharimu kiasi cha takribani shilingi bilioni 11.2 na kusema Serikali itaendelea kushughulikia changamoto za kisekta zinazoikabili wilaya hiyo hususan elimu, afya na maji.