Wakala wa Maji Vijijini RUWASA Mkoani Kagera wamepanga kuanzisha mpango wa kuwasogezea huduma ya maji wananchi majumbani ili kuwapunguzia adha kubwa ambayo wamekuwa wakiipata ya kufuata maji kwenye maeneo mbalimbali.
Kauli hiyo imetolewa na Meneja wa RUWASA Mkoani humo Mhandisi Warioba Sanya wakati wa kikao cha Menejimenti ya RUWASA na Wenyeviti wa Halmashauri zote za mkoa wa Kagera pamoja na Makatibu Tawala kilichofanyiwa Februari 18, mwaka huu katika ukumbi wa Manispaa ya Bukoba.
Mhandisi Sanya alitoa kauli hiyo wakati akiwasilisha mapendekezo ya bajeti ya mwaka 2021/2022 iliyolenga kutoa mwanga wa namna walivyojipanga kuhakikisha miradi mbalimbali ya maji mkoani humo inakamilika na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
Amesema kuwa kwa sasa wameanzisha utaratibu wa kila wanapojenga mradi wanaweka sehemu ya kuwaunganishia wananchi maji majumbani huku akibainisha kuwa katika bajeti hiyo kipaumbele kikubwa ni sehemu ambayo wananchi hawapati huduma ya maji kabisa.
“Tumeanzisha utaratibu huu ili kuweza kuwaunganishia wananchi maji hasa wale watakaohitaji, kitakachofanyika ni kutafuta mita na kuwafungia bure wao wataanza kulipia pale watakapoanza kutumia maji,” amesema Mhandisi Sanya.
Aidha, Sanya ameongeza kuwa wameomba shilingi bilioni 62.4 ili kuweza kukarabati, kuanzisha upya na kuendeleza miradi mbalimbali ya maji mkoani humo.
Kwa upande wao Wenyeviti wa Halmashauri wameipongeza hatua hiyo ya RUWASA wakisema itasaidia kuondoa usumbufu kwa wananchi na itakuwa ni hatua mojawapo ya maendeleo huku wakimuomba Katibu Tawala Mkoa kuzitaka taasisi nyingine Kama TANESCO na TARURA kuwa na vikao kama walivyofanya RUWASA.