Baadhi ya Wakazi wa Mtaa wa Makatani Kata ya Lyamkena halmashauri ya Mji wa Makambako mkoani Njombe wameitupia lawama halmashauri ya mji huo kwa kuchelewa kulipa fidia ya eneo lililochukuliwa na serikali tangu mwaka 2014 kwa ajili ya ujenzi wa soko la mazao.
Wakizungumzia na Dar24 Media kuhusu kusuasua kwa utekelezaji wa mradi huo, wakazi wa mtaa huo wamesema serikali imesababisha kuongezeka kwa ugumu wa maisha kwa wakazi wa mtaa huo ambao wameathiriwa na mpango wa ujenzi wa soko hilo.
“Kuna maeneo mengine mpaka sasa hivi yameshalimwa na waliwahamisha watu wachache wengine bado, kuna eneo kubwa walilichukua watakapo jenga sheli sehemu nyingine magodauni, kituo cha polisi na hilo eneo lote bado watu hawajalipwa mpaka leo na inaonekana wamelipwa fidia wachache wengine bado,”Wamesema baadhi ya wananchi
Akifafanua kuhusu mchakato wa ujenzi pamoja na suala la fidia kwa watu waliopisha mradi huo mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Makambako, Paul Malala amesema kuwa mchakato wa kulipa fidia umeshaanza.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa mtaa wa Makatani, Samson Mkongela amesema kuwa wananchi waliacha kutekeleza miradi ya kudumu katika eneo la ujenzi wa Soko tangu 2014 kutokana na serikali kuwa na mpango na eneo hilo.