Wakazi wa kijiji cha Madihani wilayani makete mkoani Njombe wameiomba Serikali kuharakisha ukamilishaji wa ujenzi wa ghala la matunda kutokana na matunda yao yanaendelea kuozea mashambani hali inayopelekea kupata hasara.
Wametoa kilio chao wakati wa ziara ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM mkoa wa Njombe, Erasto Ngole alipofanya ziara katika kijiji cha Madihai wikayani humo.
Akizungumzia hali hiyo, Mary Kyando mkazi wa kijiji cha Madihani amesema kwa miaka mingi kilimo chao cha matunda aina mbalimbali kimekuwa kikikwamishwa na ukosefu wa soko la uhakika la matunda pamoja na mahala pa kuhifadhia na badala yake matunda yao yamekuwa yakioza shambani.
“Matunda mengi yanaharibika sana, yamerundikana chini ya miti kwa kukosa soko, kwa hiyo tukiona ghala limefikia mahari hapa, kwetu sisi ni faida kubwa sana kimaendeleo, pia limetuletea barabara,” amesema Mary.
Amesema wanaiomba serikali kuharakisha ghala hilo ili liweze kufunguliwa na kuanza kazi kwa kuwa athari kubwa wamekuwa wakiipata ya kuuza matunda yao kwa sasa.
Naye Diwani wa Kata ya Kipagalo, Reuben Mwandilava alimweleza Katibu wa Itikadi na Uenezi, Ngole kuwa wakulima wa matunda kwenye kata yake wamekosa sehemu ya kuyapeleka matunda yao na badala yake hivi sasa yanazidi kuozea shambani.
Kwa upade wake Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM mkoa wa Njombe, Erasto Ngole, ambaye pia ni mmoja wa wadau wa kilimo cha Parachichi amesema atafuatilia kwa karibu ili kasi ya ujenzi ikamilike, kwa kuwa ameguswa sana na kilio cha wananchi hao, kwa sababu pia anafahamu jinsi gani kilimo cha matunda kilivyo na manufaa ya kumuinua kiuchumi mkulima kwa sasa.
“Kwa sababu mnafanya kazi ambayo na mimi naifanya, naamini itawalipa na italeta ukombozi kwa wananchi wa Madihani nawachangieni shilingi laki tatu ili kuchochea kasi ya kilimo cha matunda,” alisema Ngole.
Katika kutekeleza Ilani ya CCM, Ngole ametembelea na kukagua utekelezaji wa ilani hiyo katika kata za Iwawa,Ipelele na Kipagalo na kuchangia fedha taslimu zaidi ya shilingi milioni moja kuunga mkono jitihada za wananchi za kujiletea maendeleo.