Wananchi mkoani Tabora wameshauriwa kutumia usafiri wa ndege za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) mara baada ya kufanyika kwa uzinduzi wa safari za Shirika hilo kati ya mikoa ya Tabora na Dar es salaam.

Ushauri huo umetolewa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Edwin Ngonyani wakati akizindua safari za shirika hilo katika mikoa ya Tabora na Dar es salaam, ambapo amesema kuwa usafiri huo utarahisisha huduma za usafirishaji abiria na mizigo katika mikoa hiyo.

Amesema kuwa kuanzishwa kwa safari hizo katika mikoa hiyo pia kutanua wigo wa biashara na kukuza uchumi kupitia sekta mbalimbali  ikiwemo ya utalii na kilimo.

“Naamini wananchi wa mkoa wa Tabora na mikoa ya jirani, sasa mtanufaika kwa ujio wa ndege hii, matumaini yangu kwamba mtatumia usafiri huu ambao hautumii muda mrefu katika kurahisisha shughuli zenu za kibiashara na kijamii”, amesema Eng. Ngonyani.

Eng. Ngonyani amewataka wananchi wa mkoa wa Tabora kutumia fursa ya ujio wa ndege hiyo kama chachu ya kuleta maendeleo katika mkoa huo.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Sekta ya Uchukuzi, Dkt. Leonard Chamuriho, amewaasa wananchi wa mkoa huo kutumia fursa ya kupata usafiri wenye gharama nafuu na wa muda mfupi.

Naye, Mkuu wa Mkoa huo, Aggrey Mwanri, amewataka wananchi wa mkoa huo na mikoa ya jirani kujitokeza kwa wingi kupata huduma ya usafiri huo ambao walikuwa wakiusubiri muda mrefu.

 

Video: Hotuba ya Sugu yalivuruga Bunge, Waliogonganisha vyeti hawa hapa
Magazeti ya Tanzania leo Mei 6, 2017