Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauli ya Wilaya ya Ludewa Mkoani Njombe, Sunday Deogratius amewataka wananchi wa vijiji vyote wilayani humo kuhakikisha wanashiriki kikamilifu kwenye shughuli za ujenzi wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo inayoendelea katika halmashauri ya wilaya ya Ludewa.

Ametoa wito huo wakati akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Ludewa kilichopo katika Kata ya Ludewa mjini na kuwataka kushiriki ipasavyo kwenye shughuli mbalimbali za Maendeleo zinazoendelea kufanyika kijijini hapo.

Aidha, amemwagiza Mtendaji wa Kata ya Ludewa kufuatilia utendaji kazi wa mwenyekiti wa kitongoji cha Makorongoni kutokana na kushindwa kusimamia ipasavyo mradi wa ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Ludewa kijijini.

“Napongeza juhudi za uongozi wa Kitongoji cha Nyamapinda kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Ibihi iliyopo kule Nyamapinda pia kuna vijiji ambavyo bado havioneshi ushiriki wake katika shughuli ambazo Serikali imetoa pesa, naomba viongozi tusimamie ipasavyo,”amesema Deogratius

Hata hivyo, baadhi ya wananchi katika Vijiji mbalimbali wilayani Ludewa wamesema kuwa wanaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali chini ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt, John Pombe Magufuli kwa kujitolea kushiriki ujenzi na uboreshaji wa miradi mbalimbali Vijijini ambayo Serikali imetoa pesa ili kuunga mkono juhudi za Wananchi.

Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano wa SADC
Asukumwa ndani baada ya kuikosoa serikali