Wakazi wa Mitaa ya Maheve, Itulike Amani na Itulike Shuleni iliyopo katika Halmashauri ya Mji wa Njombe wanategemea kuachana na tatizo la ukosefu wa huduma ya nishati ya umeme baada ya kushuhudia zoezi la usambazaji nyaya na nguzo za umeme likiendelea katika maeneo yao.

Maheve na Itulike ni Mitaa iliyopo Jirani na mji wa Njombe lakini haijawahi kupata huduma ya umeme, jambo ambalo wananchi wa maeneo hayo walipaza sauti kuiomba Serikali isikie kilio chao kwa kipindi cha muda mrefu.

Msimamizi wa kampuni tanzu ya Tanesco (ITIDICO) inayotekeleza mradi huo Bw, Makalla Kihula amesema wanatarajia kukamilisha kazi ya kusambaza umeme katika maeneo hayo ifikapo mwishoni mwa Mwezi Octobar 2019.

Hatua hiyo inatoa matumaini makubwa kwa wakazi wa mitaa ya Maheve Itulike Amani na Itulike Shuleni ambao wamekiri kuwa itawasaidia kusonga mbele Kimaendeleo huku wakiipongeza Serikali kwa kusikiliza kilio chao na kuanza hatua za utekelezaji.

Bw, Erasto Ngole ni Mkazi wa Mtaa wa Itulike Amani pia ni Katibu wa siasa na uenezi wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Njombe amesema, alikuwa akiulizwa mara kwa mara na wananchi wenzake ni lini Serikali itamaliza tatizo hilo la kukosekana kwa nishati ya Umeme, hatua ambayo ilimlazimu kufanya ushawishi Serikalini juu ya kupata muafaka wa Jambo hilo.

Ameongeza kuwa kuwashwa kwa umeme katika mitaa ya Itulike kutawafanya wananchi wa maeneo hayo ambao wengi wao ni Wakulima wa zao la parachichi kuimarika zaidi kupitia kilimo cha zao hilo kwa kuanzisha viwanda ambavyo vinategemea nishati ya umeme.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Itulike Amani Bw, Michael Ng’ande amesema ahadi ya kupatiwa huduma ya Umeme katika eneo lake ilikuwa ya miaka mingi iliyopita lakini haikuwa na Mafanikio, Ujio wa Serikali ya awamu ya tano umewapa matumaini mapya Wananchi.

Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Oktoba 10, 2019
Singida mwenyeji maadhimisho siku ya chakula Duniani