Mkuu wa Mkoa wa Manyara Makongoro Nyerere, amesema mkoa huo umetajwa kushika nafasi ya pili kwa matukio mengi ya ukatili wa Kijinsia na kuwataka wakazi wa mkoa huo kutumia madawati ya Jinsia ili kuwafichua watu wanaofanya vitendo hivyo ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

RC Nyerere ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa Ofisi za Dawati la Jinsia na Watoto katika Kituo cha Polisi cha Orkesment Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara ambacho kimejengwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu na Afya ya uzazi (UNFPA) kwa kushirikiana na Shirika la Utu wa Mtoto (CDF).

Amesema mkoa huo unaongoza kwa mambo mazuri lakini kutajwa katika nafasi za juu kwa vitendo vya ukatili kunapaswa kukemewa ili kuondokana na nafasi hiyo ambapo amewataka Jeshi la Polisi kuzindisha mapambano katika kukomesha vitendo hivyo.

“Tumieni Dawati lililozinduliwa leo ili kukomesha vitendo hivi ambavyo vinatia aibu mkoa wet una hapa nawapongeza Jeshi la Polisi Pamoja na wafadhili waliofanikisha ujenzi wa jengo hili ambalo kwa kweli litaongeza chachu katika mapambano dhidi ya ukatili katika Wilaya ya Simanjiro”amesema RC Makongoro.

Kwa upande wake Kamishna wa Polisi Jamii Faustine Shilogile amesema ofisi hiyo ya Simanjiro inafikisha jumla ya ofisi 58 ambazo zimejengwa katika nje ya vituo vya Polisi kutokana na mwongozo wa uanzishwaji wa madawati ya Jinsia na Watoto ambao unataka mazingira rafiki yanayozingatia usiri katika kutoa huduma kwa wahanga.

Amesema mkakati wa Jeshi la Polisi ni kuendelea kutoa huduma bora kwa kuweka mazingira bora ya utendaji kazi yanayomfanya mteja anapofika kutoa taarifa aweze kuwa na amani hivyo ujenzi wa madawati hayo utaendelea kwa kushirikiana na wadau wengine wanaopinga vitendo hivyo.

Naye Msaidizi wa Mwakilishi wa  Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu na Afya ya uzazi (UNFPA) Dkt. Majaliwa Marwa amesema wamesaidia ujenzi wa ofisi hiyo ili kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia

Mbunge wa Jimbo la Simanjiro Christopher Ole Sendeka amelipongeza Jeshi la Polisi Wilayani humo kwa hatua ambazo wamekuwa wakiendelea kuzichukua kwa watu wanaofanya vitendo vya ukatili ikiwemo  vilivyotokea hivi karibuni katika Wilaya hiyo.

Waliofariki kwa mafuriko DRC wafikia 160
Iringa yapaa Kimataifa uhifadhi wa Mazingira