Wananchi wamehimizwa kujiunga kwa wingi na mfuko wa Bima ya Afya ulioboreshwa ili wapate vitambulisho vitakavyowasaidia kupata matibabu kwa mwaka mzima katika vituo vya kutolea huduma za Afya ikiwemo na Hospitali za Rufaa.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack wakati akizindua Kampeni ya kuhamasisha wananchi kujiunga na mfuko wa Bima ya Afya iliyoboreshwa katika kijiji cha Ilobashi, kata ya Masengwa, halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, ambapo amesema kuwa Bima ya Afya inawasaidia wananchi kuwa na uhakika wa matibabu kwa bei nafuu kwa mwaka mzima.
Amesema kuwa wananchi wakiwa na uhakika wa matibabu, maradhi yakiwakuta hawana fedha hawatakuwa na mawazo ya kwenda kupiga ramli chonganishi kwa sababu tayari wana vitambulisho.
Telack amewaasa pia wananchi ambao vitambulisho vyao vimekwisha muda wake walipie tena kwa mwaka huu ili waendelee kupata matibabu huku akiwakumbusha Waganga wafawidhi wa vituo vyote vya Afya kuhakikisha dawa na vifaa vinakuwepo.
“Serikali inataka Watanzania wote wanakuwa na Bima za Afya ili kuweza kutibiwa kwa wakati, ubora na kwa bei nafuu, hakikisheni madirisha ya wagonjwa wa CHF yanakuwepo na yanafanya kazi kama ilivyo kwa madirisha ya wazee,”amesema Telack
Naye Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga aliyembatana na Mkuu wa Mkoa katika uzinduzi huo, amewasisitiza wakulima wote kujiunga na mfuko wa Bima ya Afya mara tu watakapouza pamba ili wawe na uhakika wa matibabu.
“Kazi ya kilimo ina mchango mkubwa kwa pato la Taifa, asilimia 28.7 inatokana na kilimo, hivyo siku hii ni muhimu sana kwa wakulima na mimi nasema, huwezi kulima kama huna Afya nzuri” amesema Hasunga.
Wakiwahamasisha wananchi wengine kujiunga na mfuko huu, William Gwisu na Salu Izengo ambao wameshajiunga kwa muda mrefu, wameeleza kuwa mafanikio makubwa waliyoyapata kutokana na kujiunga ikiwemo kuokoa fedha nyingi baada ya kulazimika kupewa rufaa kwenye Hospitali kubwa.
Mkoa wa Shinyanga ni moja ya Mikoa mitatu nchini ambapo mradi wa CHF iliyoboreshwa umetekelezwa, mikoa mingine ni Dodoma na Morogoro. Jumla ya Wananchi 25,513 kati ya 261,608 wameshajiunga na mfuko huu tangu ulipozinduliwa rasmi Mkoani humo tarehe 4 Oktoba, 2018.