Ingawa Jumamosi iliyopita ilikuwa siku nzuri kwa mashabiki wa mpira wa miguu nchini kushuhudia mechi kati ya Timu ya Taifa (Taifa Stars) na Timu ya Taifa ya Nigeria, tukio hilo liligeuka kuwa la kisiasa huku likikiumiza Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Wananchi waliohudhuria katika uwanja huo, walionesha kutokubaliana na tangazo lililotolewa kupitia vipaza sauti vya uwanja huo lililoeleza kuwa Mbunge wa Bumbuli ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, January Makamba amewaruhusu watu wote waliokuwa nje ya uwanja huo kuingia bure.

Ofa hiyo iliyotajwa na MC kuwa ilitolewa kwa hisani ya CCM muda mfupi baada ya timu hizo kwenda mapumziko ilipokelewa kwa hisia tofauti ambapo karibu uwanja mzima ulisimama na kupaza sauti ya kauli mbiu ya Chadema, ‘people’s power’.

Licha ya kufurahia ofa hiyo, watu waliokuwa wanaingia uwanjani hapo walianza kuonesha ishara ya vidole viwili vinavyotumiwa na upinzani. Muunganiko wa sauti ulisikika wakitaja jina la mgombea wa Chadema, “Lowassa…Lowassa…Lowassa’.

Baada ya mchezo huo kumalizika huku timu zote zikiwa zimetoka sare ya bila kufungana, waandishi wa habari walimfuata January Makamba ambaye hakutaka kuzungumzia suala hilo.

“Sijui chochote, labda waulizwe TFF,” alisema Makamba.

Wananchi waliopata nafasi ya kuhojiwa na waandishi wa habari walieleza kuwa wamechoshwa na hali ya maisha magumu chini ya serikali ya CCM na kwamba mwaka huu wanahitaji mabadiliko.

“Watu wamekata tamaa, wanahitaji mabadiliko,” anakaririwa shabiki aliyejitambulisha kwa jina la Juma Hamisi.

Hivi karibuni, serikali ililikataa ombi la Chadema kutumia uwanja huo kwa ajili ya uzinduzi wa kampeni zao ambapo ilifafanua kuwa uwanja huo hauruhusiwi kutumika kwa shughuli za kisiasa.

 

Mzee Makamba Aeleza Lowassa Alivyotaka Kuikacha CCM Mwaka 1995
Magufuli Awakamia Wahandisi