Serikali imetolea ufafanuzi malalamiko ya baadhi ya watu wanaodai kukerwa na tabia ya polisi kuwaachia huru mara kwa mara watuhumiwa mbalimbali wa matukio ya kihalifu ambao ni waraibu wa matumizi ya dawa za kulevya.
Wakizungumza na @dar24news baadhi ya wakazi wa Morogoro Mjini, wamesema imekuwa ni mazoea polisi kuwakamata waraibu hao na kisha baada ya siku mbili au tatu unawaona tena mitaani kitendo kinachowakera wakazi hao.
Akijibu madai hayo Kamishna wa Tiba na Kinga wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya,Dkt Peter Mfisi amesema sheria inatambua kuwa uraibu ni ugonjwa hivyo hukumu pekee ni kumpeleka mraibu hospitali na siyo jela kama jamii inavyofikiria.
Ameongeza kuwa jeshi la polisi limekuwa likitumia weledi mkubwa wanapowakamata waraibu wa dawa za kulevya ambapo hushirikiana na familia zao kuwasainisha matibabu ya lazima ya kuondokana na uraibu kwa muda wa miezi sita, lakini wengi wao wamekuwa hawafuati adhabu hiyo na kurudi kwenye matumizi ya dawa hizo haramu.
Hata hivyo Kamishna Dkt. Mfisi amefafanua kuwa adhabu hiyo ni kwa wale waraibu wanaokamatwa na makosa ya kukutwa wakitumia dawa hizo na siyo wale wanaokamatwa wakifanya uhalifu mwingine baada ya kutumia dawa za kulevya.
“Kwa hao wengine wanaokamatwa kwa tuhuma za wizi au kumdhuru mtu,sheria huchukua mkondo wake kama kawaida ila nafikiri wakati mwingine Polisi hutumia busara na kulazimika kuwaachia kutokana na hali zao kiafya kushindwa kuhimili kukaa mahabusu kwa muda mrefu hususani wanapopatwa na arosto” Amesema Dkt Mfisi.