Wakazi wa kijiji cha Malelei Katika kaunti ya Lamu nchini Kenya kwa sasa wanalazimika kulala kwenye miti licha ya kuwa na nyumba zao.
Wakazi wa kijiji hicho ambacho kinapatikana katika wadi ya Witu wanalazimika kulala kwenye miti kwa hofu ya kushambuliwa na wanamgambo wa kundi la kigadi la Al-Shabab.
Kwa mujibu wa ripoti za mashuhuda, wakazi hao wanatumia muda wa mchana kuwa makwao na kufanya kazi zao za nyumbani kama vile ukulima na giza linapoingia wanakimbia kujificha kwenye miti.
Katika mashambulizi ya hivi majuzi, wanamgambo wamekuwa wakishambulia maboma ya wakazi na kuwaua kikatili wengi wa wahasiriwa wakiwa wanaume.
Matukio hayo yameshuhudia zaidi ya watu 15 wakiuawa na zaidi ya nyumba 15 kuteketezwa ambapo Januari 10, 2022, iliarifiwa kuwa watu wawili waliuawa na nyumba kadhaa kuteketezwa kufuatia shambulizi liliotekelezwa katika kijiji cha Salama, Kaunti ya Lamu.
Wakazi wa Juhudi, Salama na Widhu eneo la Majembeni, katika Kaunti ya Lamu walilazimika kukesha kwenye baridi kufuatia majibizano makali ya risasi hali iliyosababisha wengine kutoroka kutoka maboma yao, wakiamua kujisitiri usiku huo katika shule zilizoko karibu, idadi nyingine katika soko la Kibaoni na wengine hata kukesha vichakani.
Shambulizi hili linajiri siku chache tu baada ya wavamizi kumimina risasi kadhaa na kusababisha wakazi wa Mejembeni kutoroka eneo hilo.
Januari 3, wavamizi waliokuwa wamejihami kwa silaha zikiwemo panga na bunduki, waliwauwa watu sita na kuteketeza nyumba kadhaa kabla ya kutoroka eneo la Widhu Majembeni, kaunti ya Lamu.
Kwa mujibu wa Kamishna wa Kaunti ya Lamu Irungu Macharia, mmoja wa wahasiriwa aliuawa kwa kupigwa risasi, mwingine akakatwa hadi kuaga dunia huku wengine wanne wakiteketezwa wakiwa katika nyumba zao.
Awali, iliripotiwa kuwa shambulizi hilo lilitekelezwa na wanamgambo wa kundi la kigaidi la Al Shabaab waliosemekana kuonekana katika msitu wa Boni.
Hata hivyo, Inspekta Jenerali wa Polisi Hilary Mutyambai alifafanua kuwa uchunguzi uliashiria shambulizi hilo kuchochewa na mizozo ya shamba miongoni mwa masuala mengine.