Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze leo Septemba 15, 2016 ametoa matokeo ya utafiti uitwao ‘Rais wa Watu? Tathmini na matarajio ya wananchi kwa serikali ya awamu ya tano’ ambapo matokeo hayo yanatokana na takwimu zilizokusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,813 kutoka maeneo yote Tanzania Bara (Zanzibar haihusiki kwenye matokeo haya) kati ya tarehe 4 Juni na tarehe 20 Juni 2016.
Eyakuze amesema kuwa Wananchi wanakubali hatua zinazochukuliwa na serikali mpya inayoongozwa na Rais Dk. John Pombe Magufuli, hususani kuhusu uondoaji wa wafanyakazi hewa, sera ya elimu bure na usimamishwaji wa watumishi wa serikali kutokana na makosa mbalimbali.
Amesema Wananchi wana mitazamo chanya kuhusu utendaji wa serikali ya awamu ya tano pamoja na Rais Magufuli mwenyewe kufuatia taarifa kutoka kwa Wananchi kuwa watumishi wa umma kwenye maeneo mbalimbali wanawajibika zaidi na kwamba wamegundua kuwa kuna maboresho kwenye huduma za umma.
Hata hivyo wananchi wana mashaka kuhusu utaratibu unaotakiwa kufuatwa. Kwa mfano, wanataka udhibitisho wa vitendo viovu upatikane kwanza kabla ya watendaji kuwajibishwa, kulaumiwa ama kutiwa aibu. Vilevile wana mashaka kuhusu maamuzi ambayo yanaweza kugharimu fedha zao, kama kuzuia uingizwaji wa sukari. Hii inaonyesha kuwa wananchi hawatakuwa wakikubaliana na vitendo vyote vinavyofanywa na Rais bila kuhoji. Wananchi wanaendelea kuthamini  misingi ya utawala bora unaozingatia sharia zilizopo,” – Aidan Eyakuze
Katika ripoti hiyo Twaweza imeeleza kuwa:-
 • Asilimia 69 ya Wananchi wametaja uondoaji wa wafanyakazi hewa kama juhudi mojawapo ya Rais John Pombe Magufuli, wanayoifurahia sana,
 • Asilimia 67 wametaja elimu bure na
 • Asilimia 61 wametaja usimamishwaji wa watumishi wa serikali.
Wananchi wametaja vitendo ambavyo hawakubaliani navyo,
 • Asilimia 32 wametaja kuzuiwa kwa uagizwaji wa sukari kutoka nje pamoja na bei elekezi ya sukari, huku
 • Asilimia 58 hawapingi kitendo chochote cha Rais,

Kufuatia ripoti hiyo Twaweza wameeleza kiwango cha kukubalika kwa Rais Magufuli kwa silimia 96 ya wananchi, ambapo kiwango hicho kinaendana na viwango vya kukubalika kwa Marais wa Tanzania waliopita.

Twaweza wamesema kuwa wananchi wameeleza kukosa taarifa za kutosha kuhusu masuala muhimu ya kitaifa ambapo asilimia 4 pekee wanaosema wanapata taarifa za kutosha kuhusu masuala ya siasa nchini na asilimia 9 wamesema wanapata taarifa kuhusu masuala yanayohusu afya na elimu.
Hivyo, taarifa za maboresho yanayosemwa kuhusu huduma za umma yanatokana na uzoefu binafsi au kutoka vyanzo visivyo rasmi. Wananchi wanatamani kupata taarifa kutoka katika sekta ambazo zinagusa maisha yao kama masuala yanayohusu afya, elimu, maji na barabara yalijitokeza kama mambo muhimu. Kwa upande wa Rais Magufuli, wananchi wawili kati ya kumi (asilimia 18) wangependa kumuuliza kuhusu suala la mfumuko wa bei kwa bidhaa mbali mbali.

Serikali ya awamu ya tano imetajwa kuleta maboresho kwenye huduma nyingi za umma, Mamlaka ya Mapato Tanzania imeongoza ambapo asilimia 85 ya wananchi wamesema huduma zimeboreshwa chini ya serikali mpya.

 • Huduma ni nzuri mashuleni (asilimia 75),
 • Vituo vya polisi (asilimia 74),
 • Mahakamani (asilimia 73), vituo vya afya (asilimia 72) na
 • Mamlaka za maji (asilimia 67).
 • Watumishi wa umma wanaotoa huduma, kama madaktari, walimu, pamoja na maofisa tawala wa umma wamekuwa wakiwajibika zaidi (asilimia 95).

Twaweza wamesema kuwa takwimu ni mitazamo na maoni ya wananchi kuhusu huduma za umma na siyo lazima ikawa ndiyo hali halisi ya mabadiliko kwenye huduma hizo.

Asilimia 47 ya Wananchi wanamfahamu au wameshazungumza na viongozi wao wa vijiji, wilaya na kitaifa. Na karibu wananchi wote (asilimia 96) waliripoti kumfahamu Afisa Mtendaji wa Kijiji chao na karibu nusu yao (asilimia 47) walikuwa wameshawahi kuzungumza naye. Hatahivyo, asilimia 21 ya wananchi wanamfahamu Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya yao na asilimia 4 pekee wamezungumza naye.

Pamoja na kiwango kikubwa cha kukubalika kwa serikali ya awamu ya tano na Rais John Pombe Magufuli, wananchi wapo makini na kanuni za demokrasia na haki na wanataka zifuatwe.

 • Wananchi nane kati ya kumi (au 80%) wanasema watendaji wa umma waondolewe pale tu panapokuwepo udhibitisho wa vitendo viovu.
 • Asilimia 75 wanasema kuwa watendaji waondolewe pale wanaposhindwa kufanya kazi zao na siyo wanaposhindwa kufuata maagizo ya Rais. Pamoja na shauku yao juu ya uondoaji wa watumishi wa umma, wananchi wana maoni tofauti kuhusu matokeo ya kuwaondoa watumishi wa umma. Japokuwa asilimia 90 wanasema uondoaji wa watumishi hawa utawafanya watumishi wengine kuepuka vitendo viovu,
 • asilimia 37 wanasema itawapunguzia morali watumishi wengine.
 • Asilimia 48 wanasema uondoaji wa watumishi utawasababishia watumishi kutafuta njia mpya za kuficha maovu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Eyakuze pia amesema kuwa jambo muhimu kuhusu matokeo haya ni kuwa matarajio ya wananchi yamebadilika. Kipindi cha nyuma kulikuwa na hali ya kutokujali miongoni mwa wananchi, uzoefu uliotokana na utendaji duni uliodidimiza matarajio yao, na matokeo yake yakichangia utendaji usioridhisha kuendelea. Lakini mabadiliko tunayoyaona hivi sasa yanaonyesha kuwa utendaji wa sekta ya umma unaweza kuimarika. Wananchi wanaweza kutarajia viwango vya juu zaidi kama utaratibu huu mpya ni wa kudumu.

Wizara ya Mambo ya Nje kufanya matembezi kuchangia waathirika tetemeko la ardhi
Serikali yatoa tamko kuhusu ongezeko la fedha za mkopo vyuo vikuu