Baadhi ya wananchi  ambao wanaoishi katika maeneo ya migodi,wamelalamikia fidia wanayopewa kutoka kwa wawekezaji, na kudai kuwa hailingani na ardhi iliyochukuliwa.

Miongoni mwa migodi hiyo ni Accacia-Buzwagi ulioko kahama mkoani shinyanga ambapo viongozi wake wanaeleza kuwa wamekuwa wakijihusisha na shughuli za miradi ya kimaendelo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara, hospitali, shule na kulipa kodi inayotumiwa kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.

Lakini pamoja na shughuli zote hizo kufanyika katika eneo hilo bado baadhi ya wananchi wanaozunguka mgodi huo wanalalamikia uwepo wa mgodi huo katika kijiji chao.

”..Nina majuto kwanini nimezaliwa Tanzania na kwanini nizaliwe karibu na mgodi hapa Mwendakulima,  Kwa sababu mpaka sasa tunapata shida kupata maeneo ya kulima, kwa mfano baba yangu alilipwa milioni saba kwa ekali 23, na ilikuwa mwaka 2008,  hivyo mimi kama mimi siwezi kusema kwamba tumenufaika na mgodi huu kwa sababu bado nina maumivu..” Alisema  Simon Mabumba.

Aidhaa kwa upande wake Mwanasheria kutoka Shirika la kutetea haki za Binadamu “SHIHUDA” Pius Mpunda alisema kuwa  malipo waliyopewa wananchi  si ya haki. Kwa kuwa Buzwagi imewafidia kwa kuwajengea nyumba za chumba kimoja, alichofananisha sawa na Msalani. Akisema kuwa maendeleo ya mji huo, hayalingani na faida ambayo mgodi huo wanayopata.

Kwa upande wake, Vicent Ndesekio, Afisa mtendaji wa kata eneo hilo amesema licha ya Mgodi huo kuwajengea wananchi nyumba nzuri tofauti na walizokuwa nazo awali, bado hawaridhiki.

Aliongeza kuwa kwa sasa wanachofanya ni kubadili mtazamo kwamba mgodi unawajibika kuwafanyia kila kitu, kwani nao pia wanapaswa kujiajiri ili waweze kujitegemea.

Hata hivyo Meneja wa mgodi huo Asa mwaipopo,, amesema kwa upande wao wamefuata taratibu zote za kisheria.

”…Ni kweli kwamba mgodi huu ulipoanza kujengwa ulichukuwa baadhi ya maeneo yaliyokuwa yakimilikiwa na wenyeji. Utaratibu wa fidia ni utaratibu wa kiserikali na ni utaratibu wa kisheria. Ukiwa unafanya kazi na watu wengi kiasi uelewa na tafsiri hutofautiana, lakini utaratibu ulizingatia sheria na taratibu na ulizingatia soko ndio maana wengi waliridhika na wakalipwa. Na kama wangekuwa na madai ya msingi sidhani kama suala hili lingechukua miaka mingi kama hivi”Alisema Meneja huyo.

Kiongozi Wa Boko Haram Ajeruhiwa Vibaya Katika Shambulio Lililofanywa Na Jeshi La Nigeria
Chama Tawala Africa Kusini Chabwagwa