Polisi nchini Zimbabwe imesema inafuatilia taarifa zinazosambaa mtandaoni juu ya biashara ya ununuzi wa vidole vya miguu ya watu inayodaiwa kufanywa na duka la Ximex Mall la jijini Harare.
Msemaji wa Naibu Kamishna wa Polisi nchini humo Paul Nyathi amesema taarifa hizo zimezua taharuki na inadaiwa baadhi ya watu wameonesha nia ya kutaka kukata vidole vyao hivyo wanafuatilia na watatoa taarifa.
“Haijathibitika bado lakini inadaiwa kuna raia wanataka kukatwa vidole vya miguu ili wapate pesa na wengi wao inasemekana wanataka wapewe kabla ya kukatwa tunafuatilia,” amesema Nyathi.
Mei 28, 2022 mmiliki wa mtandao wa kijamii wenye jina la Gambakwe alichapisha habari inayoelezea uwepo wa biashara ya kuuza vidole inayoendelea katika duka kuu la Ximex Mall lililopo nchini Zimbabwe.
Baada ya chapisho hilo gazeti la burudani la H Metro la nchini Kenya likachapisha taarifa ya mahojiano na wafanyabiashara wa duka hilo ambao walisema taarifa hiyo ni.ya uzushi na ilisambazwa kwa utani.
Hata hivyo taarifa hizo zikaenea zaidi kwani chombo kimoja cha habari kiitwacho Ripples Nigeria cha nchini Nigeria kikatoa taarifa kuwa Raia wa Zimbabwe wanaripotiwa kukatwa vidole vya miguu ili wapate pesa za kujinusuru na gharama kubwa za maisha za nchini mwao.
“Hatua hiyo inatokana na uzalishaji wa bidhaa nchini Zimbabwe kudorora sambamba na uwepo wa uhaba wa fedha za kigeni zinazotumika kuagiza malighafi kutoka nje,” ilisema Ripples Nigeria.
Mtandao mwingime wa Naija News ukafafanua kuwa ipo video iliyowekwa kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter ikionesha mwanamume akichechemea huku akiwa amefunika sehemu ya kidole chake cha mguu kilichokatwa.
“Alikuwa akijigamba kwa kutumia pesa alizopata kwa kuuza kidole cha mguu na kwamba tayari alikwisha kununua gari ila.madai haya hayajathibitishwa,” ilifafanua sehemu ya taarifa ya Niger News.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo bei za vidole ambazo bado hazijathibitishwa ni dola 10,000 kwa kidole kidogo cha mguu, dola 25,000 kwa kidole cha kati, huku bei ya kidole kikubwa ikiwa ni dola 40,000.
Mfumuko wa bei chini Zimbabwe umepanda hadi kufikia asilimia 131.7 ukitajwa kuwa ni wa juu zaidi tangu kuanza kwa mwezi Juni 2021 ukichangiwa na uwepo wa vita kati ya Urusi na Ukraine.